Idadi ya watu waliofariki kwenye ajali ya basi mkoani Kagera imeongezeka na kufikia saba, ambapo wengine wawili walifariki wakiwa hospitali.
Akizungumza na www.eatv.tv, Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera Agustino Olomi amesema mpaka jana jioni ilivyotokea ajali watu watano ndio walikuwa wamefariki, lakini mpaka sasa wengine wawili wameongezeka na kufanya idadi kufikia saba.
Ajali hiyo imetokea katika kijiji cha Kasharazi wilayani Ngara mkoani Kagera, ambapo moja ya basi kati ya mabasi manane yaliyokuwa yamebeba wakimbizi yakiwa kwenye msafara sambamba na magari mengine madogo, kufeli breki na kugonga basi lingine, na kusababisha kumgonga muendesha baiskeli na kufariki papo hapo, kisha basi hilo kupinduka na kusababisha vifo vya watu wanne hapo hapo.
Kamando Olomi amesema mpaka sasa hawajajua idadi ya majeruhi kwani wakimbizi hao ambao walikuwa wakitokea kwenye kambi ya Nduta Wilayani Kibondo mkoani Kigoma na kuelekea Burundi, kupelekwa kwenye kambi ya wakimbizi karibu na eneo hilo, na wahusika wa kambi ndio wanahusika na taarifa zao.