Jide na ishu ya kuishi Nigeria


MEI 20, mwaka jana ndani ya Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar, nilibahatika kuwa miongoni mwa waalikwa katika tamasha kubwa la muziki lililotambulika kama Naamka Tena lililoandaliwa na mwanamuziki mkongwe wa kike wa Bongo Fleva nchini, Judith Wambura ‘Lady Jaydee’ ukipenda waweza kumuita Komando.

Hamu kubwa ya kuwepo katika tamasha hilo ni kumshuhudia akiimba wimbo wake ambao ulikuwa gumzo kwa kipindi hicho wa Ndi Ndi Ndi. Nilishangaa ukumbi wote ukilipuka kwa shangwe huku wengi wakiomba wimbo huo urudiwe zaidi ya mara nne.

Jide alikuwa Jide kweli, uwezo wake wa kulitawala jukwaa kwa zaidi ya miaka 15 niliushuhudia ‘live’, na ukija kwenye suala la pumzi yaani kuimba mfululizo bila kuchoka ni komando hasa, ana swagga, anajua ku-baunsi kwa kufuata midundo na jinsi ya kuimba na mashabiki.

Ukiachana na hilo, juzikati nilipata bahati ya kukutana naye na kuzungumza mengi kuhusiana na muziki akiwa kama mkongwe pekee wa kike aliyefanikiwa kuwa na albamu saba hadi sasa ambazo ni Machozi (2000), Binti (2003), Moto (2005), Shukrani (2007), The Best of Lady Jaydee (2012), Nothing But The Truth (2013) pamoja na Woman (2017).

Katika makala haya anafunguka mengi zaidi; Showbiz: Wasanii wengi wamekuwa    wakitoa albamu kwa mwaka huu huku wengine wakiwa kwenye mipango hiyo, vipi kuhusu wewe una mpango wa kuongeza nyingine ya nane?

Jide: Ujue albamu ni kitu ambacho nimekuwa nikitoa miaka yote na hadi sasa tayari nina albamu saba hivyo nitatoa tu.

Showbiz: Ni changamoto zipi unapitia ukiwa kama mkongwe kwenye muziki wa Bongo Fleva?

Jide: Changamoto ni zilezile za kila siku na hazina tofauti sana, kwenye changamoto hakuna ukongwe wala upya. Changamoto ni changamoto tu.

Showbiz: Wasanii wengi wa kike wanakuja kwa kasi kwenye gemu, ukiwa kama mkongwe kwa sasa Bongo?

Jide: Namkubali sana Lady Jaydee kuliko wasanii wengine wa kike wote Tanzania, ila pia namuheshimu sana Khadija Kopa na Patricia Hillary.

Showbiz: Vipi kuhusu Machozi Band ndiyo imekufa kabisa maana hatuisikii tena?

Jide: Siku hizi hakuna Machozi Band kuna The Band na ndio huwa inapiga kwenye shoo zote za Lady JayDee.

Showbiz: Una mpango ya kumiliki bendi tena kwa maana ya kuongeza wigo?

Jide: Bado niko na bendi na watu walewale niliokuwa nao tangu hapo awali sina mpango mwingine kwa sasa.

Showbiz: Hivi ulishawahi kufikiria kumiliki lebo ya muziki?

Jide: Anacheka! (Hapana kwa kweli).

Showbiz: Swali la uzushi. Ulishawahi kufikiria kuishi nchini Nigeria?

Jide: Kwenda na kurudi lakini sio kuishi moja kwa moja kabisa, kwani asilimia kubwa ya maisha yangu nimeyajenga Tanzania. Ila lolote linawezekana pia ikibidi.

Showbiz: Umekuwa mbali na skendo na ndiyo mmoja wa wakongwe wenye sifa hiyo nini siri yake?

Jide: Ni kwa sababu Jaydee huwa sio mtu wa skendo, sio kwamba najiepusha ila sina. Hivyo ndivyo nilivyoumbwa tu!

Showbiz: Ikitokea umepata nafasi ya kuongea na Rais John Magufuli, utamwambia nini?

Jide: Naweza nisijue hata cha kumwambia kusema kweli, huwa najiweka mbali kuzungumzia siasa na wanasiasa kwa ujumla.

Showbiz: Mwisho kabisa, mashabiki watarajie kipi baada ya ujio wako mpya wa Anaweza?

Jide: Waendelee ku-enjoy Anaweza kwa sasa!

Showbiz: Nimeona taarifa kuwa unajipanga kuzindua wimbo wa Anaweza ukiwa na mkongwe wa Reggae kutoka Jamaika, usiku huo utakuwa kama ule wa Naamka Tena wa mwaka jana?

Jide: (Anacheka!) Itakuwa nzuri sana siwezi kusema zaidi ya mashabiki kuja wao kujionea pale Golden Tulip, Machi 31, mwaka huu Golden Tulip.

Showbiz: Asante sana Jide!

Jide: Asante na wewe pia karibu tena.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad