Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira imesusia kupokea taarifa ya Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido), huku ikitoa onyo kwa wateule wa Rais John Magufuli kutekeleza wajibu wao ipasavyo na kwa kasi inayohitajika.
Agizo hilo limetolewa leo Machi 15, 2018 mkoani Singida ambapo kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Suleiman Sadiq walipofika kutembelea viwanda kadhaa mkoani humo na mwenyeji wao alitakiwa kuwa ni Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage.
Akizungumzia leo, Sadiq amesema kamati ya Bunge inapotembelea anapaswa kuwapo waziri, naibu waziri au katibu mkuu, lakini “tumemkuta naibu katibu mkuu na maofisa wengine wa wizara na wale wa Sido, ambao hawakuwa wamejindaa na tumeikataa taarifa yao.”
Amesema Mwijage alipaswa kuwapo wameelezwa amekwenda Morogoro kuhudhuria ufunguzi wa kiwanda cha Sigara eneo la Kingolwira.
“Kwa sasa tupo tu tunatembea tembea hapa Singida, lakini tuseme hawa watendaji wa Rais Magufuli wanapaswa kujitambua na kutekeleza wajibu wao. Kama wameshindwa kutoa ushirikiano kwetu hata kwa kumtuma naibu waziri (Stella Manyanya) au katibu mkuu, hii Tanzania ya viwanda kweli itakuja kama hakuna ushirikiano,” alihoji Sadiq.
Sadiq ambaye ni mbunge wa Mvomero amesema, “tumsaidie Rais Magufuli na sisi katika taarifa yetu tutajua kipi cha kufanya tutakaporudi Dodoma, kwa hiyo sisi kama wabunge hatujapenda kilichotokea leo.”