Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harisson Mwakyembe (Mb) ametangaza rasmi kanuni mbili za Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya Sura namba 306 ya mwaka 2010, katika gazeti la Serikali namba 133 (GN.No.133) na 134 (GN.No.134) zilizochapishwa tarehe 16/03/2018.
Kanuni za Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Habari za Mtandaoni) ya mwaka 2018 ijulikanayo kama The Electronic and Postal Communications (Online Content) Regulations, 2018 zimetangazwa kupitia Tangazo la Serikali Namba 133 (GN.No.133).
Kanuni nyingine ni Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Utangazaji katika Redio na Runinga) ya mwaka 2018 ijulikanayo kama The Electronic and Postal Communications (Radio and Television Broadcasting Content) Regulations, 2018 ambazo zimetangazwa kupitia tangazo la Serikali namba 134 (GN.No.134).
Kanuni hizi kwa pamoja zimetengenezwa chini ya Kifungu cha 103 cha sheria ya EPOCA na zimetiwa saini na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe ambaye ndiye mwenye dhamana na Maudhui ya Habari na Utangazaji.
Kwa ujumla kanuni hizi zinalenga kuongeza ufafanuzi wa mambo muhimu katika Sekta ya Habari, kwa ajili ya kuongoza vyombo vyenye mamlaka ya kusimamia pamoja na kurahisisha utekelezaji kwa watumiaji mbalimbali wa huduma ya Sekta hiyo.
Mchakato wa kuandaa Kanuni hizi ulihusisha wadau mbalimbali wa Habari wakiwamo wamiliki wa vyombo, watoa huduma za mawasiliano ya mtandaoni, watumiaji wa mtandao, waandishi wa habari, pamoja na wanaharakati na watetezi wa haki za walaji wa huduma za sekta hii pamoja na Wizara ikisaidiana na wataalamu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Kanuni za Maudhui ya Utangazaji wa kwenye redio na kwenye runinga pamoja na mambo mengine zimefafanua juu ya dhana kuu mbili ambazo zimekuwa katika mijadala ya watoa huduma na watumiaji wengi, mambo hayo ni kuhusu Chaneli ambazo ni lazima kubebwa na anayemiliki miundombinu ya kurushia matangazo hata kama hazijalipiwa kwenye king’amuzi cha mlaji wa mwisho ( free to air channels).
Aidha, Kanuni zinawaelekeza wamiliki wa mitambo ya kurushia matangazo kulazimika kurusha hewani Chaneli ya umma (must carry public broadcaster channel) pasipo chombo cha umma kinachorusha chaneli hiyo au mwananchi anayemiliki king’amuzi kulipia chochote.
Vilevile Kanuni hizo zimeeleza juu ya taratibu za utoaji wa leseni za maudhui kwa vyombo vya habari, aina za leseni, masharti ya utoaji wa maudhui kwa vyombo vya habari, masharti ya urushaji vipindi, masharti ya jumla kwa leseni za huduma za maudhui.
Pia, Kanuni hizo zimeeleza juu ya viwango vya kitaalamu na kiufundi katika huduma za utangazaji, utoaji wa vibali vya ujenzi wa miundombinu ya utangazaji, aina za huduma na leseni za maudhui, wajibu wa vituo vya umma, wajibu wa vituo vya kibiashara, wajibu wa vituo vya kijamii, wajibu kwa utangazaji wa maudhui yanayolipiwa pamoja na masharti kwa kampuni za miundombinu ya maudhui.
Kanuni hizi pia zimezingatia kuwalinda watoto dhidi ya maudhui yasiyofaa, muda kwa vipindi ambavyo watoto hawaruhusiwi kuona kama vile utangazaji wa maudhui yenye vitendo vya ngono au maudhui yanayoonesha vurugu.
Mambo mengine ni masharti ya kutangaza mwenendo wa Mahakama au Bunge, masuala ya uchaguzi, masharti ya kutangaza maudhui kwa watu wenye mahitaji maalum, masharti kwa utangazaji wa vipindi vya mahojiano, lugha ya kutumia katika utangazaji.
Zimeelezea pia juu ya utangazaji wa maudhui ya ndani ya nchi na vipindi vyenye maslahi ya Kitaifa, vipindi vya taarifa za kiuchunguzi au masuala ya watu binafsi (Faragha), Utangazaji wa vipindi vya moja kwa moja.
Vilevile kumewekwa utaratibu wa kupokea na kusikiliza malalamiko ya walioathiriwa na habari za mtandaoni pamoja na adhabu kwa wanaofanya makosa kupitia mawasiliano ya mtandaoni.
Kanuni hizi zitafanya kazi chini ya Kamati ya Maudhui ambayo nayo imeundwa chini ya Sheria hiyo. Wadau mbalimbali wa vyombo vya habari na utangazaji pamoja na watumiaji wa mawasiliano ya habari kwa njia ya mtandao wanashauriwa kuzipitia kanuni hizo na kuzisoma kwa kina ili kuelewa mambo yaliyofafanuliwa.
Kanuni hizi zinapatikana katika Tovuti ya Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo (www.habari.go.tz) kisha ingia sehemu ya machapisho bofya kipengele cha Sera, sheria na kanuni, pia waweza kutembelea tovuti ya TCRA (www.tcra.go.tz)
Habari Wakuu,
ReplyDeletePoleni na majukumu
samahani Naomba kuuliza kidogo
Nauliza Channel za YouTube zinazotakiwa kujisajili na TCRA ni zile zinazohusiana na masuala/Maudhui ya habari pekee?
Pili vipi na wale ambao wanatumia YouTube kupost Video/Tutorials ambazo hazihusiani na Masuala/Maudhui ya Habari kama vile
Technology, Mazoezi ya Viungo , Mapishi, Lifestyles(Vloggers) n.k
Nao wanatakiwa Kusajiliwa?
AHSANTE.