Kenya, Tanzania Wahakiki Mpaka wa Kimataifa

Kenya, Tanzania Wahakiki Mpaka wa Kimataifa
Timu za watalaamu wa upimaji ardhi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Tanzania na taasisi za usimamizi wa Ardhi nchini Kenya zimekutana wilayani Tarime mkoani Mara kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa kazi ya kuhakiki na kuimarisha mpaka wa Kimataifa baina ya nchi hizi mbili.

Mapema mwezi Machi, Naibu Waziri wa Adhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula alitangaza azma ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanza kuimarisha mipaka yake kwa nchi jirani za Kenya na Uganda baada ya ziara yake ya kukagua mpaka wa Tanzania na Kenya katika Mbuga ya Wanyama ya Taifa ya Serengeti iliyopo mkoani Mara.

Hatua ya uhakiki na uimarishaji wa alama za mipaka ya mikataifa inatokana na mpaka huu kuwa wa siku nyingi na haukuwa wazi katika maeneo mengi pia baadhi ya alama hizo kuharibiwa, kung’olewa au kuchakaa na hivyo kusababisha Serikali pande zote kushindwa kusimamia kwa ufanisi shughuli za mipakani, rasilimali za nchi pamoja na ulinzi na usalama.

Katika uimarishaji wa alama hizo za mipaka hivi sasa, kutaongezwa alama mpya ndogo zinazoonana kwa umbali wa mita 100 pamoja na kubainisha eneo la ardhi huru kwa kila upande wa nchi (buffer zone).

Wataalam wa masuala ya upimaji ardhi pamoja na maafisa mbalimbali kutoka katika ofisi za Serikali za nchi zote mbili waliojumuika pamoja wilayani Tarime mkoani Mara kupanga namna ya kutekeleza kazi ya uhakiki na uimarishaji wa mipaka ya kimataifa kwa pamoja. Wa tatu kutoka kulia (walioketi) ni Mkuu wa Msafara wa wataalam kutoka Tanzania Bw. Huruma Lugala na kulia kwake ni Mkuu wa Msafara kutoka Kenya Bw. Julius Rotich.

Mkuu wa zoezi la Uhamasihaji katika kazi ya kuhakiki na kuimarisha mipaka ya Kimataifa kati ya Tanzania na Kenya Bw. Raymond Bagenda kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi akizungumza wakati wa kikao cha pamoja cha wataalam wa masuala ya upimaji ardhi kutoka katika ofisi za Serikali za nchi zote mbili. Kikao hiko kilichofanyika wilayani Tarime mkoani Mara kinapanga namna ya kutekeleza kazi hiyo kwa pamoja. Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Rais nchini Kenya inayohusika na Usimamizi wa Mipaka ya Kimataifa (KIBO) Bw. Joseph Rotich.

Baadhi ya Wataalam wa masuala ya upimaji ardhi pamoja na maafisa mbalimbali kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na katika ofisi zingine za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakifuatilia mazungumzo kuhusu namna ya kutekeleza kazi ya uhakiki na uimarishaji wa mipaka ya kimataifa kati ya Kenya na Tanzania.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad