Kesi ya uhujumu uchumi kwa kutoboa bomba la mafuta inayomkabili mfanyakazi mstaafu wa Shirika la Mafuta Tanzania na Zambia (Tazama), Samwel Nyakirang'ani(63) na wenzake sita imeshindwa kuendelea.
Kesi hiyo ya namba 1 ya mwaka 2018, imeshindwa kuendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya hakimu anayesikiliza shauri hilo, Thomas Simba kutokuwepo mahakamani hapo.
Wakili mkuu wa Serikali, Peter Maugo amedai leo Alhamisi Machi 8, 2018, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wakati shauri hilo lilipokuja kwa ajili ya uamuzi wa dhamana.
Mbali na Samwel, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Nyangi Mataro( 54) mwalimu wa shule ya msingi Ufukoni na mkazi wa Kisiwani Mkajuni Kigamboni.
Wengine ni mfanyabaishara, Farijia Ahmed (39) mkazi wa soko Maziwa Kigamboni, Malaki Mathias (39) mkazi wa Magogoni, Kristomsi Angelus(25) mkazi wa Soko Maziwa, Fundi Ujenzi Pamfili Nkoronko(40) mkazi wa Tungi Kasirati na Hunry Fredrick (38) mkazi wa Tungi Kigamboni.
Kwa pamoja washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka matatu ya uhujumu uchumi kwa kujiunganishia isivyo halali bomba la mafuta ya dizeli, kinyume cha sheria ya uhujumu uchumi.
"Mheshimiwa Hakimu, washtakiwa wote wapo hapa Mahakamani na kesi imekuja kwa ajili ya uamuzi wa dhamana dhidi ya washtakiwa na upande wa Jamhuri tupo tayari kuendelea, "amedai Maugo.
Baada ya maelezo hayo, Hakimu Shaidi amesema hakimu anayesikiliza shauri hilo hayupo na hivyo aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 22, 2018 itakapokuja kwa ajili ya uamuzi, kama washtakiwa hao watapata dhamana au la.
Awali, Februari 15, 2018 upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Agustine Kusalika uliwasilisha maombi ya dhamana dhidi ya washtakiwa hao katika mahakama hiyo.
Katika shtaka la kwanza, inadaiwa tarehe tofauti kati ya mwaka 2015 hadi Januari 8, 2018 katika eneo la Tungi Muungano wilayani Kigamboni washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kujiunganishia bomba la mafuta ya dizeli lenye upana wa inchi moja kutoa katika bomba kubwa lenye upana wa inchi 24, bila kuwa na kibali kutoka Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA)
Maugo amedai katika shtaka la pili ambalo ni kuharibu miundo mbinu, inadaiwa kuwa siku na tarehe isiyofahamika kati ya mwaka 2015 hadi Januari 8, 2018 katika eneo la Tungi Muungano washtakiwa walitoboa na kuharibu bomba la mafuta ya dizel lenye upana wa inchi 24 ambalo lilikuwa likitumika kufirisha mafuta mali ya TPA.
Katika shtaka la tatu, inadaiwa kuwa siku na tarehe isiyofahamika kati ya mwaka 2015 hadi Januari 8, 2018 katika eneo hilohilo, washtakiwa kwa pamoja walitoboa na kuharibu bomba la mafuta mazito (crude oil) lenye upana wa inchi 28 ambalo lilikuwa likitumika kusafirisha mafuta ghafi mali ya TPA.
Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Januari 16, 2018 na kusomewa mashtaka yanayowakabili.
Hata hivyo, washtakiwa hao hawakutakiwa kusema chochote mahakamani hapo kutokana na mashtaka yanayowakabili kutokuwa na dhamana.