Kocha wa Simba: Yanga kutufikia kipointi kwetu wala halijatupa hofu yoyote

BAADA ya Simba kutoka suluhu na Al Masry kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika jana na kutupwa nje ya michuano hiyo, hatimaye wamesema kuwa sasa ligi ndiyo itakuwa tamu. Simba jana walikuwa wanatakiwa kupata ushindi au sare ya zaidi ya mabao 2-2, lakini waliambulia suluhu kwenye mchezo ambao walionyesha kiwango cha juu sana nchini Misri.

Pamoja na kuondolewa kwenye michuano hiyo, pia Simba wamekuwa na hasira zaidi baada ya kulingana kwa pointi na watani wao wa jadi Yanga ambapo kila moja ina pointi 46, hivyo wamesema kuwa hasira zao sasa ni kwenye ligi. Benchi la ufundi la Simba chini ya kocha wake mkuu, Pierre Lechantre limeweka wazi kuwa halina hofu hata kidogo na kwamba sasa mambo ndiyo yameanza kunoga.

Simba kwa muda mrefu walikuwa ndiyo vinara wa ligi kabla ya Yanga kuwafikia na timu zote kwa sasa kuwa na pointi 46, lakini Simba wenyewe wameendelea kuwa kileleni kutokana na tofauti ya mabao ya kufunga ambayo wao wanayo mengi 11 zaidi ya wapinzani wao hao.

Kocha msaidizi wa Simba, Masoud Djuma ameliambia Spoti Xtra, kuwa; “Yanga kutufikia kipointi kwetu wala halijatupa hofu yoyote ile zaidi ya kwamba wametuongezea changamoto ya kupambana zaidi kwenye kila mchezo wetu ili kupata matokeo mazuri kutafuta nafasi ya kuwatoka na kuendelea kuongoza ligi.”

“Kwa kitendo ambacho wamekifanya Yanga kwa sasa ni kunogesha tu ligi yaani limekuwa tamu zaidi kwa sababu tunalingana pointi na hivi ndivyo inavyotakiwa kuwa, lakini ikumbukwe wao wapo mbele yetu kwa mechi moja zaidi jambo ambalo utaona linatubeba sisi,” alisema Djuma.

Katika mchezo huo uliochezwa mjini Port Said nchini Misri, Simba kama wangepata ushindi dhidi ya Al Masry walikuwa wanapewa kila mchezaji shilingi milioni 5, hivyo wamepoteza dodo nono.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad