Kunguni Wawatesa Wakazi wa Mbeya Waita Mganga wa Kienyeji Ili Kuwaondoa

Kunguni Wawatesa Wakazi wa Mbeya Waita Mganga wa Kienyeji Ili Kuwaondoa
WANANCHI wa Kata ya Igurusi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, wamechangishana fedha kwa ajili ya kumlipa mganga wa kienyeji ambaye walimuita ili awasaidie kuondoa kunguni katika makazi yao miongoni mwa wadudu wengine.


Mbali na kunguni, wananchi hao wamedai kuathiriwa na viroboto na chawa kwenye makazi yao wakiamini wadudu hao wamepelekwa hapo kishirikina.

Zoezi hilo hata hivyo limewagawa wananchi hao katika makundi mawili, baadhi wakiunga mkono na wengine kupinga kwa sababu ya imani za dini.

Mgongano huo umepelekea kuwapo kwa viashiria vya uvunjifu wa amani katika kata hiyo, kumfanya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla, kuingilia kati na kupiga marufuku zoezi hilo.

Makalla alisema yeyote atakayebainika kuliendeleza zoezi hilo atachukuliwa hatua za kisheria.

Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara ulioitishwa na mkuu huyo wa mkoa jana, wananchi hao walidai kuwa waliamua kuchangishana fedha hizo na kumuita 'rambaramba' huyo baada ya kukithiri kwa matukio ya "uchawi".

Mmoja wa wakazi wa kata hiyo, Pilu Ibrahimu alisema wanashindwa kuishi vizuri kwenye nyumba kutokana na kukithiri kwa wadudu hao ambao hawajulikani walikotoka.

Alisema utitiri huo wa chawa, kunguni na viroboto uliwafanya kumuita mganga ili awasaidie kuwaondoa.

Alisema sangoma huyo aliitwa kwa nia njema na kwamba hakuna mtu aliyelazimishwa kuchanga fedha lakini zoezi likaharibika baada ya Mkuu wa Wilaya, Reuben Mfune, kupiga marufuku na kuagiza mganga huyo aondoke.

“Tunaomba turuhusiwe kuendelea na zoezi letu," alisema Ibrahimu. "Nyumba zetu zimejaa kunguni ambao hawafi kwa dawa yoyote ile.

"Rambaramba wetu alikuwa na msaada mkubwa maana walianza kupungua lakini baada ya kukatazwa tunaendelea kuumia.”

Naye Benard Mwambusi aliwatupia lawama wazee wa mila katika kata hiyo pamoja na viongozi wa dini kwa madai kuwa matukio mengi yamekuwa yakitokea lakini hawajawahi kukemea na kwamba ndiyo maana yanaendelea.

Alisema kumekuwa na matukio ya wanawake kuuawa wakiwa porini wanatafuta kuni na kisha kutelekezwa hukohuko pamoja na watoto kupotea katika mazingira ya kutatanisha.

Hata hivyo, akitoa tamko la serikali, Mkuu wa Mkoa Makalla alisema ni marufuku kwa mtu yeyote kuendeleza ushirikina katika kata hiyo na kwamba endapo watakamatwa sheria itachukua mkondo wake.

Alisema matukio kama hayo ni ya kuchonganisha watu na hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kupotea kwa amani, hivyo akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa hawezi kukubali hilo litokee.

Makalla alisema hata kwa bahati mbaya hawezi kuruhusu watu kuamini uchawi katika mkoa wake hivyo akamwagiza Mkuu wa Wilaya hiyo kusimamia na kuhakikisha zoezi hilo haramu linaendelea.

“Mimi sasa hivi naelekea Dodoma kikazi, sasa nikiruhusu zoezi hilo ambalo ni kinyume na sheria za nchi sitafika hata Iringa, nitakuwa nimeshatumbuliwa na rais," alisema Makalla.

"Ni marufuku kuendelea... kila mtu apambane na hali yake.”
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad