Kuongeza Muda Madarakani ni Ushetani- Nape Nnauye

 Kuongeza Muda Madarakani ni Ushetani- Nape Nnauye
Wakati hoja ya kuongeza muda wa Rais kukaa madarakani kutoka miaka mitano hadi saba ikionekana kufifia, mbunge wa Mtama, Nape Nnauye ameibuka na kusema hatua ya baadhi ya viongozi wa Afrika kuongeza muda madarakani ni ushetani.



Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Nape ameandika kuwa ni lazima ushetani huo upingwe kwa nguvu zote hasa na vijana, kabla haujaota mizizi na kusambaa.

Alipoulizwa jana, Nape ambaye amewahi kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kabla ya kuvuliwa wadhifa huo na Rais John Magufuli alikiri kuwa Twitter hiyo ni yake ingawa hakuwa tayari kufafanua zaidi.

Mwishoni mwa mwaka jana, Mbunge wa Chemba (CCM), Juma Nkamia ndiye aliibua hoja ya kuongeza muda wa Rais kukaa madarakani akiahidi kuwasilisha muswada binafsi bungeni wa kufanya marekebisho ya Katiba ili kufanya uchaguzi mkuu wa Tanzania kufanyika baada ya miaka saba badala ya mitano ya sasa.

Kwa mtazamo wake, Nkamia anaamini kuwa kufanya uchaguzi kila baada ya miaka mitano ni gharama kubwa kwa nchi maskini kama Tanzania na kwamba katika kipindi cha miaka mitano, nchi imekuwa na uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu na hivyo kufanya gharama za uchaguzi kuwa kubwa.

Anasema kutokana na hilo, Serikali badala ya kushughulikia kero za wananchi imekuwa ikishughulikia kutafuta fedha za maandalizi na uchaguzi.

Nkamia alisema inawezekana kufanya uchaguzi wote (Serikali kuu na Serikali za mitaa) kwa pamoja kama wafanyavyo Wakenya kwa kuwa na maboksi mengi wakati wa uchaguzi, badala ya kutumia gharama mara mbili kwa kipindi kimoja.

Hata hivyo, baadaye Nkamia alituma taarifa kwa vyombo vya habari kuwa ameondoa kwa muda hoja hiyo lakini siku chache baadaye hoja hiyo iliibukia Zanzibar baada ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutaka muda huo uongezwe na kuungwa mkono na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd akisema si wazo baya.

Hata hivyo, hoja hiyo ilijibiwa na Rais John Magufuli baada ya mazungumzo yake na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alipowataka wanachama wa CCM na umma wa Watanzania kuupuuza mjadala huo kwa kuwa haujawahi kujadiliwa katika kikao chochote cha chama na kwamba ni kinyume na katiba ya CCM na Katiba ya nchi.

Polepole akirejea mazungumzo hayo alibainisha kuwa Rais Magufuli hana mpango wowote na hatarajii kuongeza kipindi cha urais wakati wote wa uongozi wake.

Kauli ya Nape iliungwa mkono na Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Benson Bana akisema ni ya hekima na busara.

Alisema viongozi wa Afrika wanapaswa kujua kuwa wananchi wamechoshwa na vitendo vya unyanyasaji, kung’ang’ania madaraka na kujilimbikizia mali.

Bana ambaye ni profesa wa Sayansi ya Siasa alitoa mfano wa kilichotokea Zimbabwe kuwa ni mgogoro wa kiutawala na kusababisha mdororo wa kiuchumi uliotokana na Rais Robert Mugabe kusababisha nchi hiyo kutengwa kwa kuwafukuza Wazungu nchini humo na kusababisha wananchi kukosa mahitaji muhimu.

Alisema viongozi wa Afrika wanapaswa kujifunza kuwa wawapo madarakani hawana budi kutekeleza demokrasia ya kweli na kutojihusisha na vitendo vya rushwa lakini pia kutoa haki sawa na kuwaonya waliotia pamba masikioni na kujifanya hawaoni kinachoendelea:

“Tunashuhudia matendo ya majirani zetu Uganda kwa Rais Yoweri Museveni na DRC kwa Joseph Kabila. Viongozi wanapaswa kujifunza kwa haya yanayotokea katika nchi nyingine, wasitangulize masilahi yao,” alisema.

Akizungumza kwa simu, Nkamia alisema hoja yake ipo palepale na kwamba kwa sasa anaendelea na mashauriano na viongozi wake wa chama kuona ni kwa jinsi gani ataiwasilisha.

“Wakati nimeleta hoja ile mwenyekiti wangu wa chama Taifa hakuipenda na kusema tuachane nayo lakini nikuambie tu tunaendelea na mashauriano na viongozi wangu wa chama kuona ni jinsi gani nitaiwasilisha; kama nilivyosema awali simlengi Rais aliyepo madarakani,” alisisitiza Nkamia.

Hata hivyo, Nkamia alisema anamshangaa Nape kudhani kuwa wanaong’ang’ania madaraka ni viongozi wa Afrika pekee.

“Hii ni kansa kubwa kudhani mambo ya Wazungu ni sahihi, badala ya hiyo anayosema yeye wakati hata wao wana mambo yao mengi ambayo hayaridhishi,” alisema Nkamia.

Alitoa mfano wa Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Tony Blair na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel ambao wameongoza kwa vipindi zaidi ya viwili na kumtaka Nape kuacha kufikiri Afrika pekee ndiyo inafanya hivyo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad