Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kufanyia kazi changamoto zilizoibuliwa na wadau wakati wa uchaguzi mdogo wa ubunge Kinondoni na Siha bila kujali udhaifu katika uwasilishaji wa changamoto hizo.
Kituo hicho kimedai kuwa kuibuliwa kwa changamoto hizo kunalenga kujenga jamii yenye haki na usawa.
Hayo yameelezwa leo Jumatano Machi 7, 2018 na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Naemy Sillayo alipokuwa akijibu hoja zilizotolewa na NEC wiki iliyopita kutokana na tamko lililotolewa na asasi za kiraia.
Sillayo amesema tamko hilo halikutolewa na LHRC bali lilitolewa na umoja wa asasi za kiraia ambao kituo hicho ni mwanachama.
Sillayo amesema LHRC inakubaliana na hoja iliyotolewa na azaki ya kutaka NEC kuboresha kanuni za usimamizi wa uchaguzi na kutovibana vyombo vya habari.
“Hilo litasaidia kutoweka mipaka kwa vyombo vya habari wakati wa kutimiza jukumu la kutoa taarifa kwa umma,"amesema.
Kuhusu mashirika kunyimwa vibali vya uangalizi wa uchaguzi Sillayo amesema jambo hilo lilipeleka butwaa kwa azaki.
"LHRC pekee ndiyo asasi iliyopewa kibali kuangalia uchaguzi, tofauti na ilivyokuwa uchaguzi wa 2015; karibu asasi 400 ziliangalia uchaguzi. Asasi ziliomba lakini majibu yalikuwa nafasi zimejaa, tunasisitiza hili liangaliwe kwenye chaguzi zijazo na kutoa muda wa kutosha wa kutuma maombi kwa asasi,"amesema.
Hoja nyingine ambayo LHRC imejibu ni utaratibu mpya uliowekwa na NEC unaowataka watazamaji kuwasilisha taarifa zao ili zikaguliwe na kuridhiwa na tume.
"Utaratibu ulioanzishwa mwaka 2015 unaondoa dhana ya asasi za kiraia kuwa vyombo huru. Utaratibu huu unalazimisha ripoti ya awali ya uangalizi iwasilishwe kwa tume na ikiri kupokea ripoti hiyo ndipo Azaki zinazoangalia uchaguzi ziweze kutoa taarifa kwa umma.
" Hata hivyo tume haijaweka muda maalumu ambao itatumia kabla ya kukiri kuipokea ripoti ya uchaguzi,” amesema.
Amesema upo umuhimu wa NEC kuzishirikisha asasi za kiraia na wadau wengine katika maboresho ya sheria, kanuni na taratibu zinazoratibu utendaji wa tume hiyo na usimamizi wa uchaguzi kwa lengo la kuimarisha demokrasia nchini.