Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amesema hatima ya mgogoro ndani ya chama hicho ipo mikononi mwa Mahakama ikiwa watashinda kesi yao iliyopo mahakamani.
Amesema hiyo ndiyo njia pekee itakayoirejesha CUF kuwa taasisi imara na chama kimoja kama ilivyokuwa awali.
Amesema kwa sasa CUF imeshindwa kushiriki shughuli za uchaguzi nje ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutokana na hujuma alizodai kufanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).
Maalim Seif ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Machi 26,2018 jijini Dar es Salaam wakati akisoma maazimio manne ya Kamati ya Utendaji ya Taifa ya chama hicho iliyokutana jana.
“Mahakama ni chombo cha haki pekee tunachotegemea. Wanaosema Mahakama inapendelea siyo kweli, tunajua mabadiliko ni makubwa, kila jaji anataka aonekane akitenda haki.”
Amedai kuwa baada ya Mahakama kuwarudishia uanachama wabunge nane waliofukuzwa na Profesa Lipumba, mawakili wao wanafuatilia kisheria ili kurejesha haki ya ubunge wa viti maalumu kwa wanachama hao.
Maalim Seif aliyekuwa ameongozana na baadhi ya viongozi, amesema kamati hiyo imewataka wanachama wake kuwatenga wasaliti wote wanaomuunga mkono mwenyekiti huyo.