Wakati uongozi unaosimamia barabara za mabasi yaendayo haraka (BRT), ukipiga marufuku magari ya wagonjwa na polisi kutumia barabara hizo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema watalazimika kuzitumia barabara hizo wakati wa dharura.
Barabara za mabasi yaendayo haraka zimejengwa kwa ajili ya kutoa huduma zake kwenye barabara za Morogoro na Kawawa.
Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari imesisitiza kuwa hakuna chombo chochote cha moto kitakachoruhusiwa kupita katika barabara hizo zaidi ya mabasi ya mwendokasi.
Akifafanua zaidi taarifa hiyo, mkurugenzi wa wakala wa mabasi hayo (Dart), Ronald Lwakatare alisema ni kweli magari ya wagonjwa hayaruhusiwi kupita katika barabara hizo mpaka ruhusa ya polisi wa usalama barabarani.
Katika kusimamia sheria za barabara hizo, alisema zipo kanuni na taratibu mbalimbali ikiwamo sheria za barabarani, halmashauri na nyinginezo.
“Ieleweke kwamba ni marufuku kutumia barabara hizo na mtu yeyote, kwani zimetengenezwa kwa ajili ya magari hayo tu na kama ikatokea likapita basi iwe ni kwa ruhusa ya polisi wa usalama barabarani ambao wao wanajua ni muda gani na sababu gani ya kuyaruhusu magari mengine yapite,”alisema Lwakatare.
Pia mkurugenzi huyo alisema tayari Rais (John Magufuli) alishatoa maagizo ya magari yafanywe nini inapobainika kutumia njia hizo na kuwataka wanachi kuwa makini ili kuepuka kuingia katika matatizo yatakayowapotezea mali na muda wao bila sababu za msingi.
Taarifa hiyo imeeleza pia kuwa magari ya vyombo vya ulinzi na usalama yanapopita katika barabara hizo, huchangia kwa kiasi kikubwa magari ya watu binafsi kufanya hivyo.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa kuanzia jana hakuna gari lolote litakaloruhusiwa kupita kwenye barabara hizo na kwamba hata magari ya wagonjwa hayaruhusiwi kwa kuwa yana utaratibu wake uliozoeleka sehemu zote duniani.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa kuna baadhi ya magari ya wagonjwa hasa yanayotokea mjini kwenda Kimara yamekuwa yakitumia barabara hizo bila kubeba abiria kwa kigezo cha kupitisha wagonjwa.
Akizungumza na Mwananchi jana, Mambosasa alisema anawaunga mkono BRT, lakini polisi itatumia barabara hizo endapo watakuwa na dharura.
“Kama hatuna dharura tutapita barabara za kawaida. Lakini tukiwa na dharura tutapita barabara zote,”alisema Kamanda Mambosasa.