Raia wa Taiwan, Han Chuan (61) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara kujibu mashtaka manne ya uhujumu uchumi ikiwamo kukutwa na mapezi ya samaki aina ya papa ndani ya meli ya uvuvi.
Chaun, ambaye ni nahodha wa meli ya uvuvi iitwayo Buah Naga 1, anadaiwa kukutwa na kilo 90 za mapezi hayo bila kuwapo kwa miili ya papa wenyewe.
Wakili wa Serikali, Simon Wankyo alidai mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Richard Kabate kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Januari 26 katika Bandari ya Mtwara.
Wankyo alidai katika shtaka la kwanza, Chuan akiwa nahodha wa meli ya uvuvi yenye usajili namba FT 333489, alikutwa na kilo hizo za mapezi ya papa, huku shtaka la pili likidai kuwa katika tarehe tofauti kati ya Novemba 25, 2017 na Januari 26 kati ya eneo la Magharibi la mikoa ya Lindi na Mtwara mkabala na Bahari ya Hindi akiwa nahodha wa meli alisababisha uchafuzi wa mazingira ya bahari kwa kuwatupa papa baharini baada ya kuwakata mapezi huku akijua kuwa ni kinyume cha sheria.
Katika shtaka la tatu anadaiwa kuwa Januari 26 alikutwa na bastola aina ya Bereta bila kuwa na leseni.
Wankyo alidai kuwa katika shtaka nne, siku na eneo hilo, mshtakiwa huyo alikutwa akimiliki risasi 10 za bastola hiyo bila ya kuwa na kibali kutoka mamlaka husika.
Hakimu Kabate alimtaka mshtakiwa kutosema chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo kisheria kusikiliza kesi za uhujumu uchumi. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Machi 27 itakapotajwa na mshtakiwa alirudishwa rumande.