Mapya Yaibuka Sakata la Abdul Nondo Polisi Dar, Iringa Watofautiana

Mapya Yaibuka Sakata la Abdul Nondo Polisi Dar, Iringa Watofautiana
Jeshi la polisi nchini limetofautiana katika taarifa zake kuhusu kupatikana kwa Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo ambapo RPC wa Iringa alisema kijana huyo alifika mwenyewe kituo cha polisi huku Mambosasa akipinga hilo.


Katika taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire Machi 8, 2018 imeonyesha kutofautiana na kauli iliyotolewa jana Machi 13, 2018 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, kamanda Juma Bwire alisema haya.

"Jana tarehe 7 mwezi wa tatu majira ya saa moja Abdul Nondo alifika katika kituo cha polisi Mafinga wilaya ya Mufindi na kuelezea kuwa ametekwa na watu wasiofahamika, jeshi la polisi mkoa wa Iringa limefungua jalada la uchunguzi ili kubaini ukweli kama alikuwa ametekwa na kama kweli alikuwa ametekwa tunaahidi kwamba sisi jeshi la polisi tukiwapata watuhumiwa sheria itachukua mkondo wake" alisema kamanda Bwire

Taarifa ya RPC wa Iringa imeonyesha kukinzana na taarifa aliyotoa jana Kamanda Mambosasa ambaye amedai kuwa Abdul Nondo hakuripoti sehemu yoyote ile na kudai kuwa walimkuta akiendelea na shughuli zake.

"Mnamo tarehe 7 Machi mwaka huu jeshi la polisi kanda Malaamu ya Dar es Salaam lililetewa taarifa kutoka polisi mkoa wa Iringa kwamba mwanafunzi huyo aliyekuwa amedaiwa kutekwa na watu wasiojulikana alipatikana mkoani humo wilaya ya Mafinga akiwa na afya njema na mwenye kujitambua akiendelea na shughuli zake na wala hakuripoti tukio lolote kabla ya kukamatwa ili kuthibitisha kile kilichokuwa kikisemwa ametekwa na watu wasiojulikana. Hakuripoti mahali popote si kwa Mwenyekiti wa Mtaa, si kwa Afisa Mtendaji wa Kata, wala kituo chochote cha polisi mkoani Iringa bali alikamatwa akiwa Mafinga akiendelea na shughuli zake" alisisitiza Mambosasa 

Mpaka sasa jeshi la polisi linaendelea kumshikilia Abdul Nondo, kwani kwa mujibu wa wakili wa mwanafunzi huyo anasema kwamba mpaka jana Machi 14, 2018 hajafanikiwa kukutana wala kuongea na mteja wake.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad