GHARAMA za matibabu za Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, tangu alipoanza kutibiwa hadi sasa zinadaiwa kufikia Sh. bilioni moja.
Akizungumza na Nipashe jana mdogo wa mbunge huyo, Vincent Mughwai, alisema kuwa gharama hizo zitaendelea kuongezeka kwa kuwa bado anaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Leuven nchini Ubelgiji.
“Wakati anatibiwa Nairobi, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alieleza gharama zimefikia Sh. milioni 700 na huko alipo gharama zake zitakuwa nusu ya fedha hizo kwa hiyo inafika kama Sh. bilioni moja ambazo watu mbalimbali wamechanga, hakuna msaada wa bunge ingawa ni haki yake kupatiwa kwa kuwa ana bima,” alisema.
Aliongezea: “Tumefanya vitu vyote walivyokuwa wanatutaka yaani bunge mara wanatuambia tuandike barua tunaandika, lakini kinachoendelea ni danadana, sitaki kuzungumza sanaa… maana kaka yangu atatoa taarifa kwa waandishi wa habari huko mkoani Arusha,” alisema.
Wakati huo huo, familia Lissu, imesema haitakachoka kulia na kulitaka Bunge kumpatia ndugu yao haki ya matibabu anayostahili kama wabunge wengine.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha jana, msemaji wa familia, Alute Mughwai, alisema, familia haitachoka kupigania haki ya ndugu yao.
Mughwai ambaye ni wakili wa kujitegemea, alisema wanataka ndugu yao apewe haki ya gharama za matibabu ambazo anastahili kupatiwa kama ilivyo kwa wabunge wengine.
Mughwai alisema familia ilipokea barua ya Bunge, Februari Mosi, mwaka huu, ikiwataarifu kupokea barua yao ya Januari ya kuwataarifu kuhamishwa kwa mgonjwa kwenda Ubelgiji toka Kenya alikokuwa akipata matibabu awali.
“Barua hii imetutaarifu kuwa Ofisi ya Bunge inawasiliana na Wizara ya Afya ambayo ilitoa madaktari watatu kwenda Nairobi kumwona Lissu ambao hawakufanikiwa, baada ya mgonjwa kuwa tayari ameshaondoka na wakiwa tayari watatujulisha, lakini sasa mwezi na siku 15 zimepita hatuna tena mawasiliano na Bunge,” alisema.
Alisema katika barua hiyo Bunge limewashukuru tu wanafamilia kwa ushirikiano wao wa dhati na kuwajulisha kuhusu Lissu alivyoondoka Nairobi.
WAWAKUMBUSHA POLISI
Aidha, alisema wanalikumbusha Jeshi la Polisi kuhakikisha linaendelea na upelelezi wa kuwakamata waliohusika.
“Sisi kama ndugu tunaamini Mungu ndiye atafunua njia zingine ili tuweze kuchukua hatua zitakazofuata baada ya kukaa na mgonjwa pamoja na kushauriana,” alisema.
“Lakini kikubwa tutafanya hilo pale tutakapoona masuala hayo mawili yamegonga mwamba,” aliongeza.
Alisema hadi sasa hakuna taarifa yoyote wamepewa kama ndugu kuhusu ulipofikia upelelezi.
Alisema awali waliomba uchunguzi huo ushirikishe taasisi za uchunguzi za kimataifa, lakini Jeshi la Polisi lilisema wasingehitaji msaada huo kwa kuwa uwezo wa kuchunguza.
“Wasiwasi wetu polisi hawana utayari wa kuchunguza tukio hili, ndio sababu wapo kimya, mpaka sasa hakuna kinachoendelea,” alisema.
UPASUAJI TENA
Akizungumzia hali ya matibabu ya Lissu huko Ubelgiji, Mughwai, alisema juzi alifanyiwa upasuaji wa mguu wa kulia ili kufanyiwa marekebisho baada ya madaktari kugundua mifupa haiungi haraka.
“Mnajua umri nao umekwenda, uponyaji wake unachukua muda mrefu, hivyo, Watanzania naomba tuendelee kumwombea ili apone haraka,” alisema.
Alisema kikubwa wanamshukuru Mungu operesheni hiyo iliyochukua saa mbili ilifanyika kwa ufanisi mkubwa na itamchukua siku saba hadi 10 akiwa amelazwa wodini.
Hata hivyo, alisema suala la lini atarudi nchini, hawana uhakika nalo wala hawawezi kulizungumzia hadi madaktari wake watakapojiridhisha kuhusu hali yake.
Aliomba watu wenye mapenzi mema waendelee kutoa michango kupitia akaunti iliyofunguliwa na Chadema hadi hapo watakapopata mawasiliano na Lissu awapatie akaunti ya Ubelgiji aliyofungua ili wanaotaka kuingiza huko wafanye hivyo huduma za matibabu ziendelee.
Aliwashukuru Watanzania wanaoendelea kujitolea na waliojitolea juu ya matibabu yake na kuzidi kuwaombea.
Lissu ambaye anaendelea kupata matibabu alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana nyumbani kwake mjini Dodoma, Septemba 7, mwaka jana wakati wa mapumziko ya mchana akitokea kwenye kikao cha Bunge.