Mbuzi wa Tambiko Aleta Kizaazaa Moshi

Mbuzi wa Tambiko Aleta Kizaazaa Moshi

Mtu mmoja aliyetajwa kwa jina la James Mallya amejeruhiwa baada ya kukatwa mapanga na kiongozi wa tambiko baada ya kumshika mbuzi wa tambiko katika msiba kwenye Kata ya Kibosho wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro.

Akizungumza leo Machi 6, 2018 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah amesema Mallya amekatwa mapanga Machi 5, 2018 baada ya kumshika mbuzi huyo aliyeandaliwa kwa ajili ya msiba na amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, mjini Moshi.

Amesema alikatwa mapanga baada ya kiongozi wa tambiko kuchukizwa na jinsi alivyokuwa akimshika mbuzi wa tambiko, kwa kuwa kitendo hicho kiliharibu utaratibu wa mila.

“Mallya ni mkazi wa Dar es Salaam alifika kwa ajili ya kushiriki msiba, akiwa msibani alikwenda kumshika mbuzi aliyekuwa amefungwa jirani ambaye alikuwa ni kwa ajili ya tambiko kwenye msiba huo,” amesema Issah.

“Alipomshika mbuzi ndipo kiongozi wa tambiko hilo jina tumelihifadhi alipomsogelea na kuanza kumkata kwa panga kichwani.”

Kamanda huyo amesema kiongozi huyo wa tambiko alipoulizwa sababu za kufanya hivyo, amesema amechukua uamuzi huo kwa sababu Mallya aliharibu utaratibu wa tambiko, kwamba kwa mujibu wa mila zao hairuhusiwi kumshika mbuzi wa tambiko.

Katika tukio jingine, mtu mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Rama amekutwa amefariki dunia na mwili wake kutupwa katika shimo la maji machafu jirani na nyumba aliyokuwa akiishi kwenye kijiji cha Oria Kata ya Kahe Magharibi wilayani Moshi.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad