Meneja wa soko la Machinga Complex Afikishwa Mahakamani na Takukuru

Meneja wa soko la Machinga Complex Afikishwa Mahakamani na Takukuru
Taasisi ya Kuzuia  na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imemfikisha katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, meneja wa soko la wafanyabiashara wadogo la Machinga Complex lililoko jijini Dar es Salaam, Nyamsukura Masondore, kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka.

Akimsomea hati ya mashtaka inayomkabili mshtakiwa huyo leo Ijumaa Machi 9, 2018, kwa Hakimu Mkazi Adelf Sachore, Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Sophia Gura amedai mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo tarehe tofauti kati ya Septemba 29 na Oktoba 7, 2014 akiwa mwajiriwa wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kama meneja wa jengo la biashara la Machinga Complex.

Sophia amedai kuwa Masondore akiwa na jukumu la kuongoza shughuli za kila siku za jengo hilo, kwa makusudi alitumia vibaya madaraka yake kwa kutoa eneo ambalo halijaidhinishwa kwenye jengo hilo kwa Umoja wa Wauza Mitumba.

Imedaiwa kufanya kwake hivyo ni kinyume na kanuni namba 12(a) na (b) za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam( Bodi ya Huduma ya Jengo hilo) na kwamba  kutokana na kitendo hicho mshtakiwa huyo alijipatia faida yeye pamoja na wengine.

Baada ya kusomewa shtaka hilo mshtakiwa huyo alikana na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wake bado haujakamilika.

Hata hivyo, wakili anayemtetea, Jamhuri Johnson ameiomba mahakama impatie dhamana mteja wake huyo na upande wa mashtaka haukuwa na pingamizi.

Hakimu Sachore ametoa masharti ya dhamana akimtaka Masondore kuwa na wadhamini wawili wenye barua na vitambulisho kutoka taasisi zinazotambulika kisheria na  pia watasaini ahadi ya Sh 5 milioni. Na kwamba barua hizo zitahakikiwa.

Kesi imeahirishwa  hadi Machi 20, 2018 kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.

Mpaka leo saa tisa alasiri mshtakiwa alikuwa bado hajakamilisha masharti hayo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad