Meya wa Jiji Ataka Watu 10 Waajiliwe Kwa Kuzika Wafu Waliokosa Ndugu

Meya wa Jiji Ataka Watu 10 Waajiliwe Kwa Kuzika Wafu Wanaokoosa Ndugu
Kama unadhani unazo sifa za shughuli za mazishi, kuna fursa hii iliyotangazwa katika Jiji la Dar es Salaam. Wanahitajika wafanyakazi 10, kazi yao ikiwa moja tu, kuzika wafu wanaokosa ndugu.

Hayo ni maagizo yaliyotolewa na Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita kwa halmashauri zote za wilaya, akizitaka kila moja kuajiri watu wawili kwa kazi hiyo.

Jiji la Dar es Salaam lina halmashauri tano za wilaya hivyo kufanya wanaohitajika kwa kazi hiyo kuwa watu 10.

Halmashauri ya jiji hubeba jukumu la kuzika wafu ambao miili yao inakosa ndugu katika kipindi cha siku 21 hospitalini.

Akizungumza jana wakati wa kikao cha robo ya tatu cha Baraza la Madiwani wa Jiji, Mwita alisema amerudia agizo hilo alilotoa katika kikao kilichopita baada ya kuona halijatekelezwa.

Aliwaambia waandishi wa habari baada ya kikao cha baraza hilo kuwa katika kikao kilichopita, walifanya mgawanyo wa majukumu wa shughuli hiyo kwa halmashauri zote na jiji, “Tulikubaliana kuwa sisi kama jiji tutatoa usafiri, sanda na dawa lakini mpaka sasa bado sijaletewa hao watu (watumishi), tufanye hima wapatikane kabla ya kikao kijacho,” alisema Mwita.

Mbali ya suala hilo la maziko ya wafu wasiokuwa na ndugu zao, kikao hicho kilijadili pia suala la mkataba wa Soko la Machinga Complex na Mwita alisema wameunda kamati maalumu kujua hatua zitakazochukuliwa endapo mkataba wa soko hilo hautapatikana.

Soko hilo lilijengwa kwa mkopo kutoka Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF)likiwa na jumla ya vizimba 4,200 vya kufanyia biashara na lilizinduliwa mwaka 2010 lakini Mwita alisema ofisi yake haina taarifa ulipo mkataba kati yake na shirika hilo licha ya kufanyika kwa jitihada mbalimbali.

“Kwa sasa siwezi kusema lolote kwa sababu tunasubiri ripoti kutoka kwa kamati maalumu iliyoundwa, lakini kabla ya hapo nimeshafanya vikao na NSSF na ofisi ya mkuu wa mkoa, havikuzaa matunda,” alisema.

“Muwe na subira ikifika Mei tutakuwa na jambo la kuzungumza juu ya mkataba wa eneo hilo kwani ripoti itakuwa tayari.”

Mkataba huo ‘umetoweka’ huku kukiwa na madai kwamba una kasoro kadhaa zikiwamo kutofahamika kwa gharama husika za ujenzi huo pamoja na kujengwa katika ukubwa usiostahili.

Awali, kupitia kamati iliyoundwa na mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ikiwa ni utekelezaji wa agizo la aliyekuwa waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene lililotolewa Aprili 19, 2016, ilibainika kuwa mbali na utata wa gharama za ujenzi, Jiji la Dar es Salaam halina uwezo wa kulipa deni hilo kwa sababu hadi lilipokabidhiwa, jengo hilo lilikuwa na deni la Sh19.7 bilioni na hadi kufikia Machi 2016, lilifikia Sh32 bilioni kutokana na riba. Mkopo wa awali uliokuwa umetolewa wakati ujenzi wake ukianza ulikuwa ni Sh12 bilioni.

Kuhusu ukubwa, inadaiwa kuwa mkataba uliosaniwa ulieleza kwamba gharama za ujenzi huo zitahusisha ujenzi wa jengo la ghorofa sita likiwa na vizimba 10,000 lakini lililokabidhiwa ni jengo la ghorofa nne na vizimba 4,200
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad