Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Said Mohamed Mtanda ametolea ufafanuzi suala la shule ya Msingi Kabwe kuita waganga wa kienyeji kutoka Kongo, ili kutatua tatizo la kishirikina linaloikabili shule hiyo.`
Akizungumza na www.eatv.tv. Mkuu wa Wilaya hiyo Said Mtanda amesema kwamba ni kweli alipokea simu kutoka kwa Mkuu wa shule hiyo kumuelezea matatizo yao hapo shuleni, na lengo walilofikia serikali ya kijiji ili kutatua tatizo hilo ambalo limekuwa likijitokeza mara kwa mara.
Licha ya hayo mkuu wa wilaya hiyo amesema yeye kama kiongozi wa serikali ni kulichukua tatizo hilo kitaalam kwa kupeleka madaktari ambao watatafuta njia sahihi ya kutibu wanafunzi hao, na sio kuruhusu mambo ya kishirikina, ingawa hawezi kuwakataza wazee wa kijiji hicho kwani anaheshimu mila zao.
“Nilipokea simu kutoka kwa mkuu wa shule hiyo akinielezea matatizo yao, akaniambia na uamuzi wa kijiji ulivyoamua, lakini mimi kama kiongozi wa serikali nitawajibika vile ipasavyo, nitapeleka mganga mkuu wa wilaya akaangalie na namna ya kuweza kulimaliza tatizo hilo, ni tatizo ambalo mara nyingi hujitokeza mara nyingi kwenye shule zetu, lakini wao kama wanakijiji na wazee na ndio wazazi, wana uamuzi wao ambao siwezi kuwakataza, suala la kuita waganga kutoka Kongo sio kweli isipokuwa wana mpango wa kufanya matambiko yao, hayo ya waganga wa Kongo halipo”, amesema Saidi Mtanda.
Wanafunzi wa kike wa shule ya msini Kabwe iliyopo Wilayani Nkasi mkoani Rukwa wanakabiliwa na tatizo la kiafya la kuanguka, kuzimia na kupiga kelele, jambo ambalo wakazi wa eneo hilo wanahisi linatokana na ushirikina, na kuamua kutafuta waganga wa kienyeji kuweza kutatua.