Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) imeeleza umma kwamba hali ya wabunge sita kutoka Zanzibar waliopata ajali ya Alhamisi mkoani Morogoro wanaendelea vizuri na matibabu katika taasisi hiyo jijini Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa taasisi hiyo Patrick Mvungi leo Machi 31, kwa njia ya simu imeeleza kwamba wabunge hao wanaendelea kupewa huduma na madaktari bingwa wa mifupa katika taasisi hiyo.
“Wanaendelea kupata huduma kutokana majeraha waliyopata kwenye vichwa, mikono, vifua na miguu. Kwa ujumla hali zao zinaendelea vizuri,” amesema.
Wabunge hao wamelazwa katika taasisi hiyo kwa ajili ya matibabu baada ya gari walilokuwa wanasafiria kutoka Dodoma kuja Dar es Salaam kupata ajali eneo la Bwawani katika barabara kuu ya Dar es Salaam-Morogoro siku ya Alhamisi saa mbili usiku.
Kabla ya kupelekwa Muhimbili, wabunge hao walipelekwa katika hospitali ya mkoa wa Morogoro kwa matibabu.
Wabunge walionusurika katika ajali hiyo ni Haji Amir Kimbe (49), kutoka Makunduchi, Hamis Ally (54), (Mkwajuni) Bagwanji May (Twaka); Makame Mashaka (46), (Kijini); , Juma Athman Hija (Tumbatu) na Masudi Ally Hamis (Makunduchi).