Mtandao wa wanafunzi nchini Tanzania (TSNP) umesema taarifa walizo nazo za nini hasa kilichomsibu mwanafunzi mwenzao, Abdul Nondo zinakinzana na zile zilizotolewa na Jeshi la Polisi baada ya kufanya uchunguzi.
Taarifa za kupotea kwa Bwana Nondo katika mazingira ya kutatanisha ziliibuka tarehe 6 Machi baada ya Nondo kutuma ujumbe kwa mmoja wa marafiki zake usiku wa manane akisema kuwa usalama wake uko hatarini.
Akizungumza na Shirika la Utangazaji la BBC Jumanne hii muda mchache baada ya kutoa ripoti yao juu ya uchunguzi, msemaji wa TSNP Helllen Sisya amesema bado wanasubiri kauli na Nondo mwenyewe ili kujua nini kilitokea.
“Sisi bado hatuamini Uchunguzi uliofanywa na polisi kwa kuwa hatujamsikia Nondo akiongea na kile tulichoelezwa na polisi mkoani Iringa na hiki tulichokisikia leo kwa polisi Dar es Salaam haviendani”, alisema Sisya.
Mtandao wa Wanafunzi Tanzania ambao ulitoa taarifa kwa Umma kuhusu kupotea kwa Abdul Nondo,hawakubaliani na taarifa hiyo ya polisi kwa kudai kuwa inakanganya,Polisi wanadai kuwa alipatikana akiendelea na shughuli zake za kawaida alipoenda kumtembelea mpenzi wake na wakati wao walipata taarifa kutoka kwa jeshi la polisi wa Iringa kuwa Nondo alifika kituoni hapo akiwa hajitambui.
Mapema leo Jeshi la polisi nchini Tanzania lilizungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa mwanafunzi wa chuo kikuu cha Dar es salaam,Abdul Nondo aliyedaiwa kupotea katika mazingira ya kutekwa ulikuwa uzushi.
Kamanda wa Polisi,Lazaro Mambosasa amedai kuwa taarifa zilizosambaa katika mitandao ya kijamii na kuzua taharuki mnamo tarehe 6,Machi kwa madai kuwa mwanafunzi huyo ametekwa na watu wasiojulikana si za kweli kwa kuwa uchunguzi wa jeshi la polisi umebaini kwamba mwanafunzi huyo alikutwa akiendelea na shughuli zake za kawaida na wala hakutekwa au kutoa taarifa kuwa ametekwa.