Chipukizi wa klabu ya soka ya PSG ya Ufaransa, Timothy Weah, ambaye pia
ni mtoto wa nyota wa zamani wa klabu hiyo na Rais wa sasa wa Liberia
George Weah amejumuishwa kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Timothy mwenye miaka 18 ametajwa na kocha Unai Emery kwenye kikosi
cha wachezaji 18 watakao safiri leo kwaajili ya mchezo wa ligi kuu ya
Ufaransa dhidi ya Troyes.
PSG inakabiliwa na mapungufu katika safu yake ya ushambuliaji
kufuatia kuumia kwa Neymar, huku pia Kylian Mbappe na Edinson Cavani
wote wakipumzishwa kwenye mchezo wa leo hivyo huenda Timothy akicheza
vizuri atajiwekea nafasi kwenye mchezo dhidi ya Real Madrid.
PSG
ina kazi ya kupanda mlima mrefu dhidi ya Real Madrid inayoongoza kwa
mabao 3-1 hivyo ni dhahiri kocha Emery anahitaji kuwapumzisha vijana
wake ili wajiandae na mechi hiyo ya jumatano ya Machi 7.
Timothy anafuata nyayo za baba yake ambaye enzi zake alichezea PSG
kwa miaka mitatu na kushinda tuzo ya Mwanasoka bora wa Dunia mwaka 1995
kabla ya kuhamia AC Milan.