Mugina: Nateseka Katika Mahabusu ya Uwanja wa Ndege Naishi Kama Mbwa

Mugina: Nateseka Katika Mahabusu ya Uwanja wa Ndege Naishi Kama Mbwa
Mwanasheria aliyejitangaza kuwa jenerali wa vuguvugu la NRM, Miguna Miguna amesema anaishi kama mbwa katika mahabusu ya polisi iliyoko kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi.

Wakili huyo, aliyewasili Jumatatu mchana akitokea Uingereza, amekataliwa kuingia nchini licha ya amri mbili za mahakama kuelekeza arudishwe nchini baada ya kusafirishwa kwa nguvu ikidaiwa anarejeshwa kwao Canada.

Chooni

Katika taarifa yake, Miguna amesema Jumatano kwamba polisi wanamshikilia “ndani ya choo finyu na kichafu bila kupewa mahitaji ya msingi ya afya na muhimu kwa maisha”.

Gazeti la Nation halikuweza kuthibitisha madai yake kwa sababu polisi wamezuia waandishi wa habari na wanasheria kumwona.

 “Wajibu maombi hawajaniletea chakula, maji na huduma ya afya na zaidi sijapewa haki ya kupata ushauri,” alisema.

Chumba kilichopo karibu na Uwanja Na 2, anadai hakifai kuishi mtu. “Sina uwezo kwenda bafuni na sijaoga tangu Jumapili ya Machi 25. Choo kilichopo hapa ninaposhikiliwa hakina maji ya bomba,” amesema katika taarifa.

“Maji yaliyopo chooni ni ya moto tu, hivyo siwezi hata kuosha uso wala kupiga mswaki.”

Mwanasheria huyo alilaani kuendelea kushikiliwa na watu aliowaita “wadhalimu”.

Miguna Miguna arejea Kenya na makeke yake



Amri ya mahakama

Jaji Roselyn Aburili Jumanne aliamuru Waziri wa Mambo ya Ndani Fred Matiang’i, Mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji Gordon Kihalangwa na Inspekta Jenerali wa Polisi, Joseph Boinett kumwachia mwanasheria huyo na wampeleke mahakamani Jumatano asubuhi.

Maofisa wengine waliolengwa na amri ya mahakama ni Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai George Kinoti, mkuu wa kikosi cha matukio ya dharura Said Kiprotich, OCPD wa JKIA na Mwanasheria Mkuu.

“Licha ya amri ya mahakama, na kama ambavyo wamekuwa wakifanya awali, wajibu maombi hawajaniachia,” alisema Miguna.

Jaji alitoa amri hiyo baada ya Miguna kupitia wanasheria wake kuwashtaki viongozi hao kwamba wanamshikilia isivyo halali.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad