Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amemuonya msanii Emmanuel Elibariki maaruifu Ney wa Mitego, kuacha kuwadanganya wasanii wenzake wasiende kujisajili Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) wakati yeye keshasajiliwa.
Ney ni kati ya wanamuziki waliofungiwa nyimbo zao zisipigwe kwenye vituo vya redio na televisheni kutokana na kukiuka sheria za maadili za utangazaji za mwaka 2005.
Nyimbo za Ney zilizofungiwa ni ‘Hapo kati patamu’ na ‘Mikono juu’ ambazo zilielezwa maudhi yake hayafai kusikilizwa na jamii.
Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari uliolenga kutangaza kuwasamehe wasanii Pretty Kind na Roma Mkatoliki waliokuwa wamefungiwa miezi sita kutojihusisha na sanaa, Dk Mwakyembe amesema tayari baadhi ya wasanii wameanza kujirekebisha akiwemo Ney aliyepeleka kazi zake mbili Baraza la Sanaa kupitiwa kabla hajazitoa.
"Tunashukuru tangu kutolewa kwa adhabu ya kufungia wasanii na nyimbo zilizokiuka maadili baadhi yao wameanza kurudi kwenye mstari akiwemo msanii Ney ambaye kapeleka nyimbo zake Basata zikahaririwe na kuonekana hazina matatizo,” alisema Dk Mwakyembe na kuongeza:
“Japo huko mtaani amekuwa akiwahadaa wenzake kwamba yeye hawezi kufanya hivyo, mwambieni aache hiyo tabia ya kuwapotosha wenzie."
Akizungumza na MCL Digital hivi karibuni, Ney alitishia kuachana na muziki kwa kile alichodai serikali ilipofikia inawapangia vitu vya kuimba.
Ney alikwenda mbali zaidi na kueleza kuwa wao ndio wanajua mashabiki wao wanataka nini na kueleza kuwa kila wimbo anaoachia hupata watazamaji wengi kwenye mtandao jambo linaloashiria ni namna gani wanamkubali.