Rafiki wa karibu wa Mai aliyeomba asitajwe jina lake alisema kuwa, pesa hizo anazodaiwa Mai zilitokana na mwanajeshi huyo kwenda kukodi gauni la harusi kwake, akawekesha shilingi laki mbili lakini hakwenda kulichukua na baadaye kutaka kurudishiwa pesa zake ambapo Mai aligoma.
“Yule mwanajeshi baada ya kutolichukua lile gauni na kwenda kukodi kwingine, kuna siku akaenda kwa Mai kudai arudishiwe pesa zake, Mai akagoma ndipo taarifa zikafika Kituo cha Polisi Kilwa Road.
“Mai naye alienda kufungua mashtaka kwenye Kituo cha Changombe, wakaitwa na kuambiwa wayamalize lakini mwanajeshi huyo amepania kumpeleka mahakamani Mai,” alisema rafiki huyo.
Baada ya habari hizi kutua kwenye dawati la Risasi Jumamosi, mwandishi wetu alimtafuta mwanajeshi huyo ambaye alikiri kumdai Mai fedha hizo na kueleza dhamira yake ya kumpeleka mahakamani.
Naye Mai alipotafutwa na kuulizwa juu ya msala huo alisema yupo tayari kwa lolote akidai kuwa ‘mjeda’ huyo amekuwa na tabia ya kutisha watu.
“Nimejaribu sana kuwa muungwana, biashara yangu siyo ya kuichezea na kutisha wafanyakazi wangu, sheria itafuata mkondo wake,” alisema Maimartha