HALI si shwari ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mkoa wa Kilimanjaro, baada ya chama hicho kuchukua hatua ya kumsimamishwa uongozi Mwenyekiti wa Baraza la Vijana, Dickson Kibona.
Kibona alisimamishwa kazi Februari 28, mwaka huu, ikiwa zimepita siku 11 tangu kufanyika kwa uchaguzi wa marudio wa kiti cha ubunge Jimbo la Siha, ambalo Chadema iliangushwa na Chama Cha Mapinduzi katika uchaguzi huo.
Taarifa kwa umma iliyotolewa jana na Katibu wa Chadema, Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa, imeeleza kuwa Kibona anasimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake.
Waraka huo kwa umma haujaeleza wazi kwamba Kibona anasimamishwa kazi kupisha uchunguzi gani.
Sehemu ya waraka inasema: “Ofisi ya Chadema Kanda ya Kaskazini, ambayo ni mamlaka ya nidhamu na uwajibishaji kwa viongozi wa mikoa, ilimwandikia barua Kibona ambaye ni Mratibu wa Bavicha Kilimanjaro, kwa mujibu wa ibara ya 6.5.2 ya kanuni za chama ya utaratibu wa kuchukua hatua ya kinidhamu sehemu ya kazi kuhusu tuhuma zinazomkabili kama kiongozi na kama mwanachama wa Chadema.”
Kwa mujibu wa maelekezo hayo ya Golugwa ambayo yanasema kwa uzito na unyeti wake, Ofisi ya Kanda imeelekeza Kibona kusimama na kupisha uchunguzi.
Imeeleza kuwa hatua hiyo ni ya kiutawala na itatoa fursa kwa kipindi ambacho Kibona ameelekezwa kwenye barua aliyopewa kujibu tuhuma kuhusu ama aachishwe uongozi au afukuzwe uanachama kwa mujibu wa ibara ya 6.3.4 (b) na (c)