Rais Dkt. John Magufuli amuagiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aitishe kikao cha Mawaziri wote ili wajadili na kutafuta majawabu hoja zilizomo katika ripoti ya CAG aliyokabidhiwa hii leo, pia na kumtaka apeleke mapendekezo ya watu anaotaka watumbuliwe.
Dkt. Magufuli ametoa kauli hiyo leo (Machi 27, 2018) wakati alipokuwa anapokea ripoti kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali, Profesa Musa Assad hafla iliyofanyika katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam.
"Kwa ujumla Waziri Mkuu nimekupa hizi 'document' kakae kikao na Mawaziri wako wote, Makatibu wakuu, Wakuu wa Taasisi mbalimbali katika kila maeneo, kila eneo likazungumziwe wazi ili hayo maeneo yasije yakajirudia tena. Ninafahamu kuna zingine utakuta zaidi miaka hata ya 20, nina uhakika mtatengeneza utaratibu wa kuzifuta ili kusudi zisije kujirudia",amesema Dkt. Magufuli.
Pamoja na hayo, Dkt. Magufuli ameendelea kwa kusema "kuna hoja nyingine za watu ni kutokana na uzembe tu wakutokujali, watendaji wetu hawataki kuzishughulikia basi waambiwe wazishughulikie. Lakini kama kutakuwepo na watu ambao ni sugu kila mwaka wanaambiwa wao, hilo nalo mlete mapendekezo kupitia kikao chako hicho kwamba ni nani tumtoe, nani akapumzike, nani akafanye shughuli nyingine".
Kwa upande mwingine, Dkt. Magufuli amewaahidi Wabunge walioshiriki katika hafla hiyo kwa kusema ataifanyia kazi orodha ambayo huwa anapelekewa kwaajili ya kupitisha uteuzi wa wenyeviti kama walivyoomba.
Nileteeni Mapendekezo ya Kutumbua Wasiofaa- Rais Magufuli
0
March 27, 2018
Tags