KIUNGO wa Simba, Haruna Niyonzima ametoa kauli za matumaini kwa mashabiki wa timu yake akisema anaendelea vizuri na matibabu ya kifundo cha mguu kilichomweka nje ya uwanja kwa miezi mitatu sasa.
Kwa wiki ya pili sasa Niyonzima yupo nchini India katika Hospitali ya Jeevika ya nchini humo, akipatiwa matibabu ya enka bila ya kufanyiwa upasuaji wa aina yoyote kama wengi walivyodhani.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Niyonzima alisema afya yake inaimarika siku hadi siku, hivyo anamshukuru Mungu kwa kuendelea kumsimamia katika maendeleo ya afya yake.
Niyonzima raia wa Rwanda aliyejiunga na Simba akitokea Yanga msimu huu, alisema kutokana na maendeleo yake mazuri ya afya anaamini siku zake za kurejea uwanjani zinakaribia.
“Kwanza nina furaha timu yangu inaendelea kufanya vizuri, halafu nina faraja kuona majeraha yangu yanaendelea, natambua Mungu anaendelea kunipa wepesi wa kupona.
“Naamini siku si nyingi nitaungana na wenzangu kwani matibabu ninayopata ni mazuri kiasi kwamba naona Mungu ni mwema sana kwangu, kwani nilijua nitafanyiwa upasuaji kitu ambacho hakijafanyika.
“Sina uhakika zaidi lakini nategemea kurudi Jumamosi (leo) kama mambo yakikaa sawa,” alisema Niyonzima.