BEKI wa kati wa Kagera Sugar, Juma Nyosso, amefunguka kuwa, kwa sasa amebakiza mechi moja tu kati ya zile tano alizotakiwa kuzikosa baada ya kusimamishwa na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), hivyo anajiandaa kurudi kuiokoa timu yake hiyo.
Nyosso alisimamishwa kucheza mechi tano za Ligi Kuu Bara baada ya kukutwa na kosa la kumshambulia shabiki wakati timu yake ya Kagera Sugar ilipokubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Simba, Januari 22, mwaka huu.
Mechi alizokosa Nyosso kutokana na adhabu hiyo na matokeo yalivyokuwa ni hizi; Kagera 1-1 Singida United, Kagera 2-1 Majimaji, Yanga 3-0 Kagera na Kagera 1-0 Mwadui. Mechi ijayo dhidi ya Ndanda, ndiyo ya mwisho.
Kagera Sugar ambayo kwa sasa inashika nafasi ya 12 ikiwa na pointi 21, imebakiwa na mechi nane ambazo inatakiwa kuzitumia vizuri ili isishuke daraja mwishoni mwa msimu huu.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Nyosso amesema: “Mechi ijayo dhidi ya Ndanda ndiyo itakuwa ya mwisho katika adhabu yangu, hivyo najiandaa kurejea kuipambania timu yangu ili tuweze kubaki ligi kuu.
“Kwa sasa hatupo kwenye nafasi nzuri, hivyo ni lazima tujipange kuhakikisha tunapambana katika mechi hizo nane zilizosalia tunakuwa salama.”