BAADA ya Simba kutolewa katika Kombe la Shirikisho Afrika, mastraika
wa timu hiyo John Bocco na Emmanuel Okwi kwa pamoja wameapa kufia
uwanjani ili Wekundu wa Msimbazi wabebe ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu
huu.
Simba iliondolewa na Al Masry ya Misri katika Kombe la Shirikisho
baada ya awali kutoka sare ya mabao 2-2 jijini Dar es Salaam halafu
ugenini wakatoka suluhu.
Kutokana na hali hiyo, Okwi na Bocco wamesema lengo lao sasa ni
kuhakikisha wanapambana kufa na kupona kwenye Ligi Kuu Bara ili waweze
kuiwezesha Simba kutwaa ubingwa.
Simba inaongoza katika ligi kuu ikiwa na pointi 46 sawa na Yanga,
inayoshika nafasi ya pili, lakini wenyewe wana tofauti kubwa ya mabao ya
kufunga na kufungwa.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Okwi alisema,
mipango yao ya kuiwezesha Simba kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho
imekwama, sasa wanaelekeza nguvu zao kwenye ligi kuu.
“Tunarudi kujipanga kwenye ligi kuu, kwani ndiyo sehemu pekee
tunapotakiwa tupambane kufa na kupona ili mwakani tuweze kushiriki tena
michuano ya kimataifa, tutapambana tuwe mabingwa,” alisema Okwi.
Kwa upande wake, Bocco ambaye pia ni nahodha wa Simba, yeye alisema;
“Kiu yangu na wachezaji wenzangu ni kuhakikisha tunatwaa taji la Ligi
Kuu Bara, maana ndiyo silaha pekee tuliyonayo kwa sasa, hiyo ndiyo
tiketi ya sisi kucheza mechi za CAF mwakani.
“Pia tunajua furaha ya mashabiki wa Simba kwa sasa ni kuona tunatwaa
ubingwa na siyo kitu kingine, hivyo tumejipanga kuhakikisha hilo
linatokea bila tatizo.”
Simba leo Jumamosi inatarajiwa kuanza mazoezi kujiandaa na mchezo dhidi ya Njombe Mji, Aprili 3, mwaka huu.