Panya Road Waibuka Wavamia Mitaa Tabata Wapora Mali

Panya Road Waibuka Wavamia Mitaa Tabata Wapora Mali
Kwa mara nyingine tena taharuki, hofu na wasiwasi mkubwa viliwakumba wakazi wa Tabata wilayani Ilala jijini Dar es Salaam kwa takribani saa tatu baada ya kundi maarufu la uporaji la Panya Road kuvamia mitaa mbalimbali na kupora mali.

Kundi hilo lililokuwa na vijana zaidi ya 30 waliokuwa wameshika nondo, visu, mapanga na bisibisi jana usiku Machi 29,2018 lilisababisha wakazi wa Tabata Kisiwani, Kimanga hadi Kinyerezi kujifungia majumbani mwao na baadhi kujifungia ndani kutokana na jinsi kundi hilo lilivyokuwa likivamia biashara na nyumba kupora.

Mmoja wa mashuhuda wa eneo la Tabata Kisiwani, Isaya Subi amesema tukio hilo lilianza saa mbili usiku ambapo kundi hilo lilivamia katika eneo hilo, kupora mali mbalimbali kwenye maduka pamoja na kuwapora wapita njia.

“Vijana hawa si mchezo walikuwa kama 30 hivi kila mmoja alibeba nondo, bisibisi, wembe na spoku wakikukuta njiani wanakupiga huku wakikusachi na kuchukua kila kitu ulichokuwa nacho wengine walivamia maduka na kuchukua bidhaa mbalimbali,”amesema Subi.

Mkazi wa Kinyerezi, Leila Lameki amesema eneo hilo walivamia saa tano usiku na kuanza kuporwa mali mbalimbali, lakini mmoja wa vibaka hao aliingia kwenye nyumba moja na alidhibitiwa na wananchi wa eneo hilo huku wenzake wakifanikiwa kutoroka.

“Kwa umoja wetu wananchi tuliweza kulidhibiti hili kundi kati ya hao mmoja alikamatwa na kuanza kupigwa na kusababishia kifo chake huku wenzake wakitimua mbio,” amesema Leila.

Kamanda wa Polisi  Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema usiku wa kuamkia leo kuna kundi lilivamia eneo la Kinyerezi na kupora mali mbalimbali, lakini kati ya wahusika mmoja aliuawa na wananchi.

Amesema polisi walifika eneo hilo na kukuta wahalifu hao wameshatoweka na kukuta silaha mbalimbali katika eneo hilo ikiwemo nondo, visu na bisibisi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad