Rais Akutana na Uongozi wa Tume ya Uchaguzi kwa Mazungumzo

Rais Akutana na Uongozi wa Tume ya Uchaguzi kwa MazungumzoRais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Shein amekutana na uongozi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kusisitiza haja ya kuendeleza umoja na ushirikiano kati ya Tume hiyo na ya Zanzibar (ZEC) ili Tanzania iendelee kuheshimiwa


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akizungumza jambo na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Semistocles Kaijage, Ikulu Zanzibar.

Dkt. Shein amesema hayo leo alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa NEC, Ikulu mjini Zanzibar ulipofika kwa ajili ya kujitambulisha ukiongozwa na Jaji Semistocles Kaijage Mwenyekiti wa Tume hiyo akifuatana na Makamu Mwenyekiti Jaji Mkuu Mstaafu wa Zanzibar Hamid Mahmoud Hamid pamoja na Mkurugenzi wa Uchaguzi Kailima Ramadhani.

Katika Mazungumzo hayo, Dkt. Shein aliupongeza uongozi huo kwa kuendeleza umoja na ushirikiano uliopo kati ya (NEC) na (ZEC) na kusisitiza haja ya kuendelezwa ili kuendelea kuijengea sifa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuendelea kufanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa.

"Ushirikiano wa pamoja utasaidia kwa kiasi kikubwa kuendeleza majukumu kwa Tume zote mbili hasa ikizingatiwa kuwa kila upande una uzoefu wake ambapo kwa Zanzibar masuala ya uchaguzi hasa wa vyama vingi yalianza tokea mwaka 1957 na baadae kuendelea hadi hivi leo. Nimevutiwa na mafanikio yaliopatikana na Tume kutokana na kutekeleza majukumu yao. vyema yakiwemo ya kuhakikisha wananchi wanatumia haki yao ya msingi ya kupiga kura, wanaendesha chaguzi, wanasimamia na hatimae wanatoa matokeo kwa wakati", amesema Dkt. Shein.


"Matumaini yangu makubwa kuwa Mwenyekiti huyo ataendeleza vyema majukumu yake kama alivyofanya Mwenyekiti aliyekuwa kabla yake Jaji Mstaafu Damiani Lubuva ambaye muda wake wa kushika wadhifa huo umemaliza kwa kutoa ushirikiano mzuri na NEC sambamba na kutekeleza vyema majukumu yake".

Pamoja na hayo, Rais Dkt. Shein amesema kuwepo kwa ofisi za kudumu NEC Zanzibar ni suala la lazima na kuahidi juhudi za makusudi zitachukuliwa na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutekeleza jambo hilo ili kurahisisha shughuli za tume hiyo.

Kwa upande wake, Jaji Semistocles Kaijage amempongeza Rais Dkt. Shein kwa kuendelea kuingoza vyema Zanzibar kutokana na ushindi mkubwa alioupata katika Uchaguzi Mkuu uliopita ambao umemuwezesha kuendelea kuiongoza Zanzibar kwa kipindi cha pili.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad