Rais John Magufuli ameifumua Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na kuanzisha ofisi mbili huru zitakazosimamia mashauri ya jinai na madai ambayo Serikali ina masilahi nayo.
Mabadiliko hayo ambayo yametangazwa hivi karibuni kupitia notisi za Serikali namba 48, 49 na 50, yameeleza muundo mpya wa ofisi hiyo kwa kuanzisha Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Jinai na ile ya Wakili Mkuu wa Serikali.
Japokuwa ofisi hizo mpya zitakuwa chini ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, mamlaka yake katika kuteua, kuadhibu na kuwasimamia maofisa na wafanyakazi wanaofanya kazi chini ya ofisi hizo yameondolewa.
Chini ya muundo mpya, AG anabaki kuwa mshauri mkuu wa Serikali katika masuala ya kisheria na kiutawala, naibu AG atakuwa mkuu wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu.
Mabadiliko hayo ni hitimisho la mchakato wa miaka mingi wa mawazo ya wataalamu wa sheria waliopendekeza kutenganishwa kwa jukumu la kusimamia masuala ya madai na yale ya jinai kutoka kwenye usimamizi wa moja kwa moja wa AG.
Masuala hayo sasa yanawekwa chini ya udhibiti wa moja kwa moja wa wakili mkuu wa Serikali na ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya jinai.
Mabadiliko hayo pia yanayaweka mambo yote ya kisheria ambayo si ya kimahakama yanayohusiana na Katiba na haki za binadamu chini ya waziri mwenye dhamana ya katiba na masuala ya sheria.
Ibara ya 36 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inampa Rais mamlaka ya kuanzisha na kufuta nafasi za madaraka ya namna mbalimbali katika utumishi wa Serikali ya Muungano.
Kwa mujibu wa mabadiliko hayo, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ndiye ataongoza Ofisi ya mkurugenzi wa mashitaka ya jinai.
Ofisi yake itachukua na kuendesha kesi zote za jinai kwa niaba ya Serikali Kuu, idara zake zinazojitegemea, wakala Serikali na Serikali za Mitaa.
Pamoja na kuwasimamia maofisa wa sheria na mawakili wa Serikali walio chini yake, DPP ataratibu na kusimamia uchunguzi wa kesi za jinai na kuendesha mashtaka ya jinai mahakamani.
Kwa upande mwingine, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali itakuwa huru na inayojitegemea mbali ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Ofisi hii imeundwa ili kuongeza uwezo wa Serikali katika kuendesha mashauri ya madai yakiwamo ya haki za binadamu na masuala ya kikatiba katika mahakama.
Kama ilivyo kwa DPP, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali itachukua na kusimamia mashauri ya jinai na upatanishi kwa niaba ya Serikali, hivyo kutoa maelekezo kwa maofisa wa sheria, mawakili wa Serikali wanaoendesha masuala ya jinai.
Mwanzoni mwa mwezi uliopita, Rais Magufuli alitoa kauli iliyoashiria mabadiliko makubwa katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na ile ya DPP baada ya kueleza kutoridhishwa ya utendaji wa ofisi hizo.
“Sitalalamika tena ninajua nitakavyofanya kwa sababu nimeshajifunza vya kutosha,” alisema Rais Magufuli alipohutubia katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini.
Alianza kwa kuwapa pole majaji kwa changamoto wanazokumbana nazo pindi wanapo shughulikia mashtaka yanayopelekwa na Serikali na kuahidi kulifanyia kazi jambo hilo kabla ya Februari kuisha.
Rais Magufuli alisema bado kuna tatizo kubwa katika ofisi ya DPP na AG ambalo wakati mwingine huwapa majaji changamoto kubwa.
“Najua mnapata shida sana mnapo-deal (mnaposhughulika) na mashtaka yanayoletwa na Serikali, mnauona kabisa ushahidi upo lakini watetezi hawajitokezi hadharani kuutetea.
“Mwaka jana nililalamika lakini mwaka huu nitalishughulikia vizuri. Sitalalamika tena ninajua nitakavyofanya kwa sababu nimeshajifunza vya kutosha na nimejua wapi kuna ‘weakness’ (udhaifu) na wala huu mwezi wa Februari hautoisha.”