Rais wa Shirikisho la soka nchini Tanzania TFF Wallace Karia leo amejitokeza mbele ya waandishi wa habari na kufafanua baadhi ya mambo yanayodaiwa kufanywa na TFF ikiwemo matumizi ya fedha kiasi cha bilioni 3.7.
Karia amesema fedha hizo zimetumika kwenye matumizi mbalimbali ya uendeshaji wa shughuli za mchezo wa soka nchini, ikiwemo Ligi mbalimbali nchini, vyama vya soka vya mikoa pamoja na malipo ya wafanyakazi na mafunzo mbalimbali.
Aidha Rais Karia ameongeza kuwa ndani ya uongozi wake amefanikiwa kulipa deni la Bilioni 1.2 ambalo alilikuta TFF ikidaiwa na TRA, Mfuko wa Jamii (NSSF) pamoja na wafanyakazi na watoa huduma mbalimbali ndani ya shirikisho.
Kuhusu wafanyakazi kutopewa ajira Karia amesema ni kweli shirikisho limepunguza idadi ya wafanyakazi kutoka 44 mpaka 21, ambao wapo kwasasa huku wengine wakiwa wanajitolea na kufanya mafunzo kwa vitendo na endapo watafikia vigezo watapewa ajira za kudumu.
Moja ya mafanikio mengine ya uongozi wake Karia amesema ni kuingiza timu 4 za taifa za soka kambini kwaajili ya michuano mbalimbali ndani ya mwezi April. Timu hizo ni Taifa Stars, Twiga Stars, Ngorongoro Heroes na Serengeti Boys.