Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela ametoa siku 14 kwa vyombo vya ulinzi na usalama Wilaya ya Korogwe mkoani humo kufanya uchunguzi na kutoa ripoti ya chanzo cha kuteketea kwa moto bweni moja la shule ya wasichana Korogwe usiku wa Machi 4, 2018.
Akizungumza mara baada ya kutembelea shule hiyo leo Machi 5, 2018 Shigela amesema ni mapema kuzungumzia chanzo cha moto huo huku akivitaka vyombo hivyo kuanza uchunguzi ili kubaini chanzo pamoja na madhara yaliyojitokeza.
“Kulitokea tatizo la umeme kuwaka na kuzima ambalo hata mkoani lilikuwepo ila hatuna uhakika, hivyo naagiza vyombo vya ulinzi na usalama kwa siku 14 kuchunguza chanzo cha tatizo na athari zake kwa wanafunzi na mali zao ili tujue,” amesema Shigella
Pia, Shigela ameagiza wadau wa elimu kuona umuhimu wa kuchangia shule hiyo kwa maelezo kuwa yanahitajika magodoro na vifaa vingine muhimu shuleni hapo ili wanafunzi waweze kuendelea na masomo yao.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Annisia Mauka amesema hakuna madhara kwa mwanafunzi yeyote kwani wakati moto unatokea wote walikuwa wanajisomea darasani.
Amesema mpaka sasa kuna bajeti ya Sh1.3bilioni kwa ajili ya ukarabati wa shule hiyo yakiwemo mabweni ila hakuna bajeti ya bati kwa ajili ya ujenzi.
Daktari wa Hospitali ya Wilaya ya Korogwe, Frank James amesema walipokea wanafunzi 43 walioonekana wazi kuathiriwa na moshi wakati bweni hilo likiwaka moto lakini walipatiwa matibabu na kuruhusiwa kurudi shuleni.