Na Baraka Mbolembole
KUELEKEA mchezo wao wa kumi wa Ligi ya Mabingwa Afrika Afrika, rekodi ya Yanga SC katika michezo tisa iliyopita ya michuano hiyo ndani ya miezi 23 iliyopita ‘haishawishi’ walio wengi kuamini mabingwa hao wa Tanzania bara wana uwezo wa kupindua matokeo ya 1-2 wakiwa Gaborone na kufuzu kwa hatua ya makundi kwa mara ya pili.
Tangu walipojaribu kwa kiwango cha juu kuwaondoa ‘wababe wa michuano’ Al Ahly kutoka Misri, April, 2016, Yanga haijapata kukutana na washindani wakubwa katika michuano ya Caf lakini bado wamekuwa wakikwama kufuzu kwa hatua ya makundi.
Mwaka mmoja baada ya kiwango cha juu jijini Cairo ambako waliondolewa katika michuano dakika ya mwisho ya mchezo, mabingwa hao wa VPL wamemudu kushinda michezo miwili tu ya mabingwa Afrika-tena dhidi ya timu kutoka Shelisheli (Ngaya Club, St. Louis) huku wakichapwa nyumbani kwa mara ya kwanza baada ya miaka nane na Watswana, Township Rollers wiki moja iliyopita.
Yanga ni wagumu na hucheza vizuri ugenini Caf
9 April, 2016 chini ya kocha Hans van der Pluijm, Yanga ililazimishwa sare ya kufungana 1-1 na Al Ahly SC katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Wengi waliamini wangeendeleza ‘mlolongo’ wa matokeo yao mabaya ugenini hasa wanapocheza dhidi ya Al Ahly na timu nyingine za Kiarabu.
Lakini kufikia dakika 90’ jijini Cairo, matokeo yalikuwa 1-1 na wakati wengi wakiamini mshindi ataenda kupatikana kwa njia ya mikwaju ya penati, wababe hao wa Misri walifunga goli la ushindi dakika za mwisho wa mchezo huo wa marejeano.
Kuanzia hapo hadi sasa, Yanga imekutana na wapinzani watatu tofauti na hawajapoteza mchezo ugenini katika michuano hiyo. Walishinda ugenini 1-5 dhidi ya Ngaya Februari, 2017 na walilazimisha suluhu dhidi ya Wazambia, Zanaco FC, Machi, 2017 licha ya kwamba waliondolewa katika michuano kwa sheria ya goli la ugenini baada ya awali timu hizo kufungana 1-1 Dar es Salaam.
Mpinzani wao wa nne tangu walipochapwa na Al Ahly miaka miwili iliyopita tayari ‘amewaonyesha shoo.’ Ni ukweli ulio wazi kuwa Yanga walichezewa mpira wa kiwango cha juu wiki moja iliyopita walipochapwa 1-2 na Rollers. Bado ninaweka imani kubwa kuwa Yanga watalipa kisasi Gaborene na si ajabu wakaacha simulizi ya ‘shoo’ watakayoionyesha.
Imani yangu inatokana na mwenendo wa timu na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja. Kiwango cha Juma Abdul katika mchezo uliopita dhidi ya Stand United siku ya Jumatatu hii, na maendeleo ya vijana kama Makka Edward, Yusuph Mhilu na urejeo wa ‘ufit’ wa Ibrahim Ajib kunatengeneza kundi jingine la wachezaji wasiotarajiwa na wapinzani. Miezi 24 iliyopita Yanga walicheza vizuri sana jijini Kigali vs APR, halafu Cairo.
Kama watakuwa na ‘msukumo wa kulazimisha kupindua matokeo’ naona wakifunga magoli walau matatu dhidi ya Township. Ni kujituma, kuamini, na kuwa tayari kimwili, kiakili, kimbinu na kiufundi. Ni mara moja tu katika washindani wao sita waliokuja Dar kucheza nao CCL, Yanga walicheza vizuri. Dhidi ya APR walicheza vibaya, angalu vs Al Ahly, ila dhidi ya Ngaya, Zanaco, St. Louis na Rollers zote wamecheza vibaya.
Mechi 5 za Yanga ugenini hivi karibuni michuano ya kimataifa, klabu bingwa Afrika (CCL) na kombe la shirikisho Afrika (CCC).
23/08/2016 CCC TP Mazembe 3-1 Yanga
12/02/2017 CCL Ngaya Club 1-5 Yanga
18/03/2017 CCL Zanaco 0-0 Yanga
15/04/2017 CCC MC Alger 4-0 Yanga
21/02/2018 CCL St. Louis 1-1 Yanga
17/03/2018 CCL Township Rollers ?? Yanga
Inasemekana ni presha ndiyo huchangia Yanga kushindwa kucheza vizuri wanapokuwa nyumbani lakini hucheza vizuri ugenini kwa sababu hawasumbuliwi na mashabiki wao wengi wanaopenda kuharakisha ushindi na kutokubali uwepo wa makosa ya kimchezo wanapocheza uwanja wa Taida, Dar.
Watoto wenyewe wa Yanga ndiyo watakaopokelewa kishujaa
Moja kati ya habari zilizovutia sana na kufuatiliwa hadi barani Ulaya-hasa nchini Uturuki mapema mwaka 2003 ni kuangushwa kwa ‘mbabe’ wa soka la vilabu barani Afrika wakati huo, Zamalek. Mahasimu hao wa Al Ahly katika soka la Misri walikuwa na mataji matano ya ligi ya mabingwa Afrika na hadi wanakutana na Simba walikuwa ndiyo mabingwa mara nyingi zaidi wa kihistoria wa ligi ya mabingwa (mabingwa mara tano)
Zamalek walikuwa wanatawala soka la Afrika huku wakiwa klabu tajiri zaidi Afrika wakati huo. Walishinda Confederation Cup mwaka 2001, wakashinda Champions league 2002 lakini mbele ya ardhi yao wenyewe walishuhudia wakiondolewa katika michuano, na kutemeshwa ubingwa ambao wameshindwa kuurudisha tena hadi sasa.
Simba ilikuwa na mchezaji mmoja tu wa kigeni wakati walipopokelewa kishujaa jijini Dar es Salaam. Mrundi, Ramadhani Wasso ambaye alitawala beki ya kushoto pekee ndiye alikuwa katika kikosi kabambe cha kocha Mkenya, marehemu, James Siang’aa (mwenyezi Mungu amrehemu) zaidi ya hao ni vijana wenyewe wa Simba walioweka historia hiyo nzuri isiyofikiwa hadi sasa.
Ilikuwa Simba ya wazawa wenye njaa ya mafanikio na wenye kuhitaji kucheza michuano mikubwa kama ligi ya mabingwa Afrika. Kwa wanasoka wengi barani Ulaya kucheza michuano ya ligi ya mabingwa ni ndoto, hivyo baada ya miaka 20 tangu kizazi cha kina Edibilly Lunyamila, vijana kama kina Kelvin Yondani wanapaswa kukumbuka kuwa hawajawahi kucheza michuano ya makundi ya michuano mikubwa zaidi Afrika hivyo wanapaswa kuwasukumu ‘yosso’ wasio na uzoefu kuhakikisha wanaichapa na kuwaondoa Rollers katika mchezo ujao ili wafike makundi.
Mechi 5 za Simba ugenini hivi karibuni michuano ya kimataifa, klabu bingwa Afrika (CCL) na kombe la shirikisho Afrika (CCC).
18/02/2012 CCC Kiyovu Sports 1-1 Simba
06/04/2012 CCC ES Setif 3-1 Simba
13/05/2012 CCC Al Ahly Shendi 3-0 Simba
03/03/2013 CCL Recreativo do Libolo 4-0 Simba
20/02/2018 CCC Gendarmerie 0-1 Simba
17/03/2018 CCC Al Masry ?? Simba
Yanga ya sasa ni tofauti sana na Simba ya 2003, lakini wana wachezaji nanne hadi tisa wazawa ambao wanaanza kikosi cha kwanza hivyo wanaweza kutumia uzalendo wao kupigana kufa na kupona kuhakikisha klabu inatinga hatua inayofuata ambayo pia itawafanya waingize zaidi ya bilioni 1.2
Kuishinda Rollers na kufuzu kwa hatua ya makundi kutawafanya vijana kama Pius Buswita, Hassan Kessy, Said Juma Makapu, Mwinyi Hajji na wenzao kupokelewa kishujaa watakaporejea nchini huku pia wakitaraji kujiuza zaidi kimpira na kuingiza pesa katika akaunti zao. Wao ndiyo Yanga, na mashujaa wanaoweza kupewa sifa kemkem baada ya matokeo yao mazuri katika dakika 90’ zijazo Caf Champions League.