WAKATI ikitarajia kuondoka nchini kesho kwenda Misri kwa ajili ya mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika, kocha msaidizi wa Simba, Masoud Djuma, amesema "dawa kubwa" ya kuhakikisha wanawafunga Waarabu na kusonga mbele ni utulivu.
Simba inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo ya SportPesa, itashuka dimbani ugenini katika mji wa Port Said Jumamosi ikiwa na kumbukumbu ya sare ya mabao 2-2 waliyoipata katika mechi ya kwanza iliyofanyika Machi 7 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na gazeti hili jana, Djuma, alisema kuwa wakiwa ugenini watacheza bila presha na endapo wachezaji wao watatulia na mipira, nafasi ya kuwafunga na kupata ushindi itapatikana mapema.
Djuma alisema kuwa kama hakuna utulivu na umakini, si wao wala wapinzani watakaoweza kuibuka na ushindi katika mchezo huo wa marudiano ambao atakayeshinda atapata nafasi ya kusonga mbele katika mashindano hayo ya kimataifa.
"Maandalizi yanakwenda vizuri na tunaamini uwezo wa kuwafunga tunao, mfumo gani tutacheza huko ni siri ya kocha mkuu, tusubiri muda na siku hiyo mtaiona timu itakavyopambana," alisema Djuma, kocha wa zamani wa Rayon Sports ya Rwanda.
Aliongeza kuwa wanawajenga wachezaji wao kuufikiria mchezo huo wa kimataifa kwanza na kusahau vita ya ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo wanapigana na mahasimu wao Yanga.
" Hakuna mechi rahisi, hakuna mashindano rahisi, tuko vitani, tunaamini sisi si wasindikizaji, tumeingia kushindana na kupambana kuhakikisha tunawapa furaha mashabiki, tunajua kiu ya Simba katika ligi na mashindano ya ndani, pamoja tuñaweza," Djuma alisema.
Wakati huo huo uongozi wa Simba umewataka mashabiki walio tayari kuongozana na kikosi hicho ili kwenda kuwashangilia katika mechi hiyo ya marudiano itakayofanyika kuanzia saa 2:30 usiku kwa saa za Misri.
"Gharama ni Dola za Marekani 500 ambazo ni kwa ajili ya tiketi ya kwenda na kurudi pamoja na viza, safari itakuwa ni Ijumaa na kurudi Dar es Salaam Jumapili," alisema Haji Manara, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba.