Sajent, Tiko Hapatoshi! Kisa Dulla Makabila Kula Mzigo kwa Mashosti Hao

Sajent, Tiko Hapatoshi! Kisa Dulla Makabila Kula Mzigo kwa Mashosti Hao
UBUYU una tabia moja ya ajabu, ukiula sana, lazima ukuchubue mdomo, lakini siku zote mlaji haachi kuumung’unya! Msanii maarufu wa miondoko ya Singeli Bongo, Abdallah Ahmed ‘Dullah Makabila’, anadaiwa kuzua kizaazaa mjini.



Jamaa huyo anadaiwa kuwachanganya vilivyo waigizaji wawili wa Bongo Movies ambao awali walikuwa mashosti, Husna Idd ‘Sajenti’ na Tiko Hassan ambapo sasa hapatoshi. Uchunguzi wa Ijumaa Wikienda ulibaini kuwa, ubuyu huo uliwahi kusambaa, lakini nyuma ya pazia bado kukawa na vita kali ya chinichini kati ya kundi la Sajenti na lile la Tiko.



Vita hiyo ilijenga ngome mbili, kila moja ikirusha maneno makali kwa nyingine. Hata hivyo, katika vita hiyo, Tiko ambaye alidaiwa kumkwapua Dullah kwa Sajenti alionekana ndiye mbaya hivyo kuuzika urafiki wao waliokuwa nao kabla ya sakata hilo.


Sajent.

MSIKIE MTOA UBUYU

Mtoa ubuyu wetu alinyetisha kuwa, ni kweli kulikuwa na ukaribu kati ya Sajenti na Tiko, kiasi cha kuvaa nguo saresare au hata kwenda kwenye sherehe mbalimbali za mjini wakiwa pamoja.

“Chanzo cha kuvurugika kwa ushosti wao ni Dullah ambaye ilisemekana alimtema Sajenti na kwenda kutuliza mtima wake kwa Tiko,” alinyetisha mtoa ubuyu wetu.



SAJENTI AFUNGUKA

Baada ya kuunyaka ubuyu huo, Ijumaa Wikienda lilianza kwa kumtafuta Sajenti. Alipoulizwa kuhusu madai ya kutemwa na mwanaume wake na kwenda kwa rafiki yake, alitema cheche;

Ijumaa Wikienda: Sajenti mambo vipi? Kuna habari ya wewe kutemwa na Dullah kisha akaenda kwa Tiko wakati ninyi mlikuwa ni marafiki, je, kuna ukweli wowote?



Sajenti: Ni kweli, aliniacha yuko kwa Tiko sasa hivi..!

Ijumaa Wikienda: Imekuwaje sasa na ninyi mlikuwa marafiki?

Sajenti: Siku zote mwenye tabia hiyo hawezi kuiacha, ndivyo ilivyokuwa.

Ijumaa Wikienda: Kwa hiyo na wewe umekubali kumuachia hivihivi mpenzi wako?

Sajenti: Mbona nimeshaanza kusahau? Nipo na ninaendelea na maisha yangu mengine kabisa.


Tiko

HUYU HAPA TIKO

Baada ya kuzungumza na Sajenti, Ijumaa Wikienda lilimtafuta Tiko na kumuuliza kuhusu tuhuma hizo ambapo naye alifunguka akionesha kuwa kuna mchezo uliofanyika kati yao.

Ijumaa Wikienda: Tiko vipi hili sekeseke linaloendelea kati yako na Sajenti kuhusu wewe kutembea na Dullah wakati ninyi mlikuwa marafiki?

Tiko: (anaguna) kwanza kwenye upande wa urafiki, sidhani kama tulikuwa marafiki kihivyo.

Ijumaa Wikienda: Vipi kuhusu kutembea na Dullah wakati ulijua wazi ni shemeji yako kwa Sajenti?

Tiko: Ukweli ni kwamba, jambo hilo anaweza kulizungumzia Dullah maana sijui hata nitaelezaje, lakini ukweli ni kwamba Dullah anajua kila kitu. Baada ya kumsikia Tiko, Ijumaa Wikienda lilimsaka Dullah ambaye naye alibanwa kugonganisha mtu na rafiki yake kwani ilidaiwa kuwa alijua wazi walikuwa ni marafiki.

Dulla Makabila.

Ijumaa Wikienda: Dullah kuna madai kuwa umemtema Sajenti na kwenda kwa Tiko ambaye walikuwa ni marafiki na ulikuwa ukifahamu hilo, je, hilo likoje?

Dullah: Ni kweli kabisa hujakosea, niko na Tiko, lakini kuna vitu vilinifanya nifanye hivyo.

Ijumaa Wikienda: Lakini si ulijua wazi walikuwa ni marafiki? Kwa nini uliamua kuchanganya au kuwagombanisha?

Dullah: Mimi nilianza kumjua Tiko kabla hata ya Sajenti, ni mwanamke ambaye alikuwa akilini kwangu na pia sioni kama kuna shida hata kama walikuwa wanajuana ilimradi mmoja nimeshaachana naye

Ijumaa Wikienda: Kwa hiyo una mpango gani na Tiko?

Dullah: Unajua mara nyingi mambo yangu nataka yawe siri ila itajulikana huko mbeleni, itoshe tu kusema kuwa ninampenda sana Tiko.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad