Akizungumza na MCL Digital leo Jumatatu Machi 26, 2018, katibu wa chama hicho, Samuel Andrew maarufu Braton amesema sakata la Diamond na naibu waziri huyo ndio sababu kuu ya kuomba kuonana na Dk Mwakyembe.
Machi 19, 2018 Diamond wakati akihojiwa na Kituo cha Redio Times cha jijini Dar es Salaam, alilaumu hatua ya Serikali kuzifungia nyimbo 15 mwezi uliopita, zikiwamo mbili za kwake.
Diamond hakuishia katika mahojiano hayo yaliyoongozwa na mtangazaji Omary Tambwe, Machi 20, 2018 kupitia mtandao wa Twitter alimjibu naibu waziri huyo akisema ametumia njia hizo kumjibu kwa kuwa naye alitumia hizo hizo.
Katika maelezo yake Braton amebainisha kwamba awali walipanga kuonana na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), kikao ambacho ilikuwa kifanyike leo.
Hata hivyo, amesema baada ya kushauriana na wenzake waliona ni vema kikao hicho akawepo na Dk Mwakyembe kwa maelezo kuwa hata Basata watapeleka taarifa za mazungumzo yao wizarani.
“Unapoongelea waziri ndio mtu wa mwisho kuongea na kutolea uamuzi wa tutakachozungumza, hivyo tukienda Basata ni kama tunazunguka tu wakati kitu tunachohitaji sasa ni utekelezaji na si taarifa,”amesema.
Alipoulizwa kama Shonza atakuwepo kwenye mkutano huo, Braton amesema hana uhakika japo vikao vingi vya wasanii huwa anakuwepo na hata hicho wangependa awepo pia.