Serikali, Airtel Zaanza Mazungumzo

Serikali, Airtel Zaanza Mazungumzo
MAZUNGUMZO kati ya kamati maalum iliyoundwa na Rais John Magufuli na kampuni ya Bharti Airtel inayomiliki hisa katika kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania yameanza rasmi jana jijini Dar es Salaam, imeelezwa.

Katika mazungumzo hayo, taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais ilisema, kamati iliyoundwa na Magufuli inaongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi na timu ya Bharti Airtel inaongozwa na Mwanasheria Mkuu wake, Mukesh Bhavnani.

"Mazungumzo hayo yana lengo la kufikia makubaliano yatakayokuwa na tija kwa pande zote mbili (Serikali ya Tanzania na Bharti Airtel) na kuimarisha sekta ya mawasiliano nchini Tanzania," ilisema taarifa ya Ikulu.

Kampuni ya Bharti Airtel iliomba kufanyika kwa mazungumzo hayo baada ya kamati iliyofanya uchunguzi kuhusu umiliki wa kampuni ya Airtel Tanzania kuwasilisha ripoti yake kwa Rais, taarifa hiyo ilisema zaidi.

Mapema mwaka huu kamati hiyo ya uchunguzi ilitoa taarifa iliyosema ubinafsishaji wa kampuni ya Airtel uligubikwa na ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu.

Januari 11, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango aliwasilisha taarifa ya kamati kwa Rais Magufuli ambaye aliagiza kufanyika kwa uchunguzi huo Desemba 20, mwaka jana.

Dk. Mpango alisema serikali imejiridhisha kuwa ubinafsishaji wa Shirika la Simu Tanzania (TTCL) kwenda Celtel, baadaye kuhamishiwa Zain na sasa Airtel ulifanyika kwa ukiukwaji mkubwa wa sheria, kanuni na taratibu.


Kufuatia ukiukwaji huo, Dk. Mpango alisema serikali inayomiliki asilimia 40 ya hisa za Airtel imeamua kufanya mazungumzo na kampuni ya Airtel inayomiliki asilimia 60 ya hisa, ili nchi iweze kupata haki yake.

“Lakini niwaambie Watanzania yale ambayo tumeyaona ni machafu sana, ni mambo ya ovyo kabisa, nchi yetu kwa kifupi tuliingizwa mkenge, ni fedha nyingi zimepotea kwa hiyo sisi katika majadiliano haya lengo letu litakuwa ni kuhakikisha Watanzania wanapata haki yao,” Dk. Mpango alisema siku hiyo.

Na sasa mazungumzo hayo yameanza, kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Ikulu.
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Sheria ndio sheria lakini Airtel imezaliwa katika misingi ya wizi wakati nchi yetu imemezwa na ufisadi, na hata huo mlolongo wa ubadilishwaji wa majina ya kampuni kutoka TTCL kwenda Celtel halafu kwenda Zain halafu kwenda Airtel? Haikuwa mabadilisho ya makosa hapana. Ilikuwa ni mipango ya kuua ushahidi. Ni sawa sawa na mtu alieba mtoto halafu akaenda kumbadilisha majina. Lakini cha kusikitisha zaidi hii ni kampuni ya serikali ambayo taasisi za serikali nyingi hutumia kwa mawasilianao, sasa vipi usalama wa nchi yetu wakakabidhiwe watu binafsi tena wageni? Dunia ya leo ina mataifa machachari sana katika kutumia nyanja za mawasilianao katika kuiba siri za mataifa mengine zanahusiana na masuala mbali mbali yawe ya biashara au siasa, yawe ya masuala ya kimaendeleo au uchumi nakadhalika nakadhalika.Na Serikali au nchi makini haiwezi kabisa kuzembea na mashirika mama yao ya mawasilianao. Unaweza kumuona muekezaji wa kihindi kumbe ni boya tu. Biashara ya mawasilianao ni sawa sawa na biashara ya makinikia ina vitu vingi vya thamani ndani yake . Au tuseme tu biashara ya mawasilianao ni muhimu zaidi kuliko makinikia kutokana na unyeti wake kunakohusiana na masuala ya usalama wa nchi. Nchi kukosa udhibiti wa vyombo vyake vya mawasilianao ni sawa na baba mwenye nyumba kumkabidhi mpangaji tena asiemjua vizuri anakotoka wapi funguo zote za nyumba mpaka za chumba anacholala yeye mwenyewe. Sasa huwezi kusema baba mwenye nyumba huyo akili zake zipo sawa sawa .

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad