SERIKALI ya Ufaransa imeipongeza Serikali ya Tanzania kwa mapambano dhidi ya rushwa na inaamini fedha zinazotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali zitatumika kama ilivyokusudiwa.
Kauli hiyo imetolewa leo (Jumatatu, Machi 05, 2018) na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Bw. Frederic Clavier alipomtembelea Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwenye makazi yake Oysterbay jijini Dar es Salaam.alozi Clavier amesema Ufaransa imeridhishwa na mapambano ya rushwa yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli wataendelea kushirikiana nayo katika uboreshaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Pia Balozi huyo amesema Septemba mwaka huu wanatarajia kufungua ofisi ya Shirika la Kimataifa la Misada ya Maendeleo la Ufaransa (AFD) jijini Dar es Salaam ili kurahisisha utoaji wa huduma. Kwa sasa ofisi za AFD zipo Nairobi nchini Kenya.Shirika hilo limekuwa likishirikiana na Serikali, katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo na ya maji safi na maji taka kwenye mikoa ya Simiyu, Mwanza, Musoma na Morogoro.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imeweka kipaumbele katika uwajibikaji na kupambana na rushwa ili kuhakikisha fedha zinazotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi zinatumika vizuri pamoja na wananchi kupata haki.
Amesema mapambano dhidi ya rushwa yataiwezesha Serikali kufikia malengo yake ya kukuza uchumi kupitia sekta ya viwanda, uwekezaji, kilimo na utalii, hivyo ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka nchini Ufaransa ili waje kuwekeza kwenye ujenzi wa viwanda, kilimo, madini na miundombinu mbalimbali.
Pia Waziri Mkuu amesema Serikali itashirikiana na Ufaransa katika kuandaa mikutano mbalimbali itakayowakutanisha wadau wa sekta binafsi kutoka nchi zote mbili ili kuwapa mbinu za namna ya kukuza uchumi.