Shilole Akutwa na Hati ya Utapeli Mahakama Yamuhukumu Kulipa Faini ya Milioni 14

Shilole Akutwa na Hati ya Utapeli Mahakama Yamuhukumu Kulipa Faini ya Milioni 14
MSANII wa Bongo Fleva, Zuwena Mohamed ‘Shilole’ amehukumiwa kulipa faini ya Tsh. Milioni 14 na mahakama ya Mwanzo Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam baada ya kupatikana na hatia ya utapeli kusababisha hasara kwa kushindwa kufika kwenye shoo.

Katika kesi hiyo iliyotolewa hukumu leo Machi 1, 2018, imethibitika kuwa Shilole alilipwa kiasi cha Tsh. Milioni tatu kwa Mary Musa kwa ajili ya kutumbuiza siku ya mkesha wa Pasaka mwaka jana 2017 katika Ukumbi wa Heineken uliopo Mbagala-Kijichi jijini Dar es Salaam lakini alishindwa kutokea kwenye shoo hiyo kama walivyokubaliana.

Kutokana na kitendo hicho,  mashabiki waliofika kwenye shoo hiyo walipandwa hasira na kufanya fujo huku wakiharibu mali ukumbini hapo hivyo kumsababishia mwandaaji ambaye ni Mary, hasara ya Tsh. Milioni 14 ambazo mahakama imeamua Shilole azilipe kama fidia kwa mlalamikaji.


Baada ya tukio hilo, Mary alifungua kesi mahakamani hapo akiomba kulipwa kiasi hicho cha fedha kama fidia ya hasara aliyoipata kutokana na Shilole kushindwa kufika lakini msanii huyo anadaiwa kupuuza wito wa mahakama.

Akisoma hukumu hiyo, hakimu wa mahakama ya Mwanzo Kinondoni, A. P. Mshingwa amesema Shilole amekuwa akitumiwa wito mara kwa mara na mahakama afike kusikiliza kesi yake lakini amekuwa akikaidi kufanya hivyo hadi mahakama ilipomuandikia wito mwingine kwenye Gazeti la Uhuru lakini hakufika pia.

Shilole aliambatana mahakamani hapo na mumewe, Uchebe,  na wakili wake ambaye baada ya kufuatwa kwa mahojiano na Global TV, alikataa kutaja jina lake wala kuzungumza chochote kuhusu kesi hiyo.

Mahakama imemuamuru azilipe pesa hizo haraka ndani ya wiki moja vinginevyo mali zake zitaanza kukamatwa.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad