Safari ya Simba kwenye michuano ya kombe la shirikisho Afrika imeishia Misri baada ya kulazimisha suluhu na wenyeji wao Al Masry katika mchezo wa marudiano uliochezwa kwenye mji wa Port Said usiku wa Machi 17, 2018.
Simba ilikuwa ikihitaji ushindi wa aina yoyote ili ijihakikishie kufuzu hatua inayofuata kutokana na sare ya kufungana magoli 2-2 katika mchezo wa awali wa raundi ya pili ya mashindano hayo.
Katika michezo minne ambayo wamecheza katika mashindano ya kombe la shiikisho Afrika, Simba imetolewa huku ikiwa haijapoteza mchezo hata mmoja.
Simba 4-0 Gendarmerie
Gendarmerie 0-1 Simba
Simba 2-2 Al Masry
Al Masry 0-0 Simba
Baada ya kutupwa nje ya mashindano hayo, Wekundu wa Msimbazi wanarejea kupambana kwenye ligi kuu Tanzania bara ambapo hadi sasa wanaongoza licha ya kuwa pointi sawa na Yanga wao wana mchezo mmoja wa kiporo.
Simba inahitaji ubingwa wa ligi ili kujihakikishia nafasi ya kurejea kwenye mashindano ya kimataifa Afrika kwa msimu ujao. Wameshatolewa kwenye kombe la shirikisho Tanzania bara (FA Cup) ambalo walikuwa mabingwa msimu uliopita wakapata fursa ya kucheza kombe la shirikisho Afrika.