Tamasha la Mwanamuziki Harmonize Lazua Gumzo Rwanda


Usiku wa kuamkia jana Jumamosi msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Harmonize alikuwa nchini Rwanda ambapo ilikuwa ni mara yake ya kwanza kutumbuiza nchini humo kwenye tamasha la uzinduzi wa lebo ya muziki ya The Mane.

Tamasha hilo ambalo limefanyika mjini Msanze liliibua gumzo nchini Rwanda baada ya kwenda tofauti na muda uliotangazwa awali.

Tamasha hilo ambalo limefanyika wilaya ya Msanze nje kidogo ya mji wa Kigali lilitakiwa kuanza saa 8:00 mchana hadi saa 12:00 lakini cha kushangaza muda huo kwenye viwanja vya tamasha kulikuwa na watu wachache huku waandaji wa tamasha wakikaa kimya bila kutoa taarifa yoyote ile.

Moja ya watu waliyohudhuria kwenye tamasha hilo ambaye pia ni mtangazaji wa kituo cha redio cha Isango FM cha Mjini Kigali, Janvier Popote amesema kuwa hali hiyo ilizua taharuki huku watu wengi nje ya viunga hivyo wakilalamika kuhujumiwa.

“Nilifika majira ya saa 9:00 mchana nilikuta watu wachache ingawaje ndio muda uliyotajwa. Kuna watu walianza kupatwa na hofu na wengine wakilalamika kuwa wamehujumiwa. Lakini cha kushangaza ilipofika saa 1:20 usiku watu wakaanza kufurika kwenye viwanja vya tamasha japokuwa muda uliyokuwa umepangwa kwa ajili ya tamasha ulikuwa umeisha,“amesema Janvier.

Hata hivyo, moja ya waandaaji wa tamasha hilo amekataa katu kuelezea sababu ya tamasha hilo kuchelewa kuanza.

kwa upande mwingine mashabiki na wadau wa muziki nchini humo wamesema kuwa tamasha hilo lilipangwa muda mbaya kwani masaa yaliyotajwa yalikuwa masaa ya kazi.

Hali hiyo pia imejitokeza kwenye show nyingine jana ambapo kama kawaida ilichelewa kuanza kitu ambacho kimezua gumzo kwa wadau wa muziki nchini humo, kwa madai kuwa mapromota wa muziki nchini Rwanda hawapo makini kwenye muda jambo ambalo linakera na linaweza kupelekea vurugu jukwaani.

Kwa upande mwingine, ilipofika saa 2:00 usiku tamasha hilo lilianza rasmi ambapo wasanii lukuki kutoka Rwanda akiwemo Marina, King James, Riderman, Christopher, Jay C, Queen Cha na wengineo.

Harmonize ndiye aliyekuwa msanii wa mwisho kupanda kwenye jukwaa hilo ambapo alitumbuiza nyimbo zake zote.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad