Tambo za Yanga, Simba Kujulikana Leo

 Tambo za Yanga, Simba Kujulikana Leo
NENO ‘tambo’ lina maana mbili. Kwanza ni jambo lililofumbika, jambo ambalo utatuzi wake haujulikani. Pili ni umbo kubwa aghalabu la mtu; jitu.

Maana zote mbili zazihusu Simba na Yanga ambazo zote zipo nnje ya nchi kwenye michuano miwili tofauti ya kimataifa. Naam, Yanga na Simba ni timu zilizoanzishwa zamani na ndizo zinazotambulika zaidi kimataifa.

Kwa mechi za kimataifa, mara nyingi Yanga imekuwa ikiondoshwa mapema, hasa na timu za Waarabu isipokuwa mara moja tu ilipofikia hatua ya nusu fainali.

Angalau Simba ilipata kutinga fainali lakini ikashindwa kutamba kwa timu ya Ivory Coast ilipofungwa mabao 2-0 mbele ya aliyekuwa Rais wa awamu ya Pili, Alhaj Alli Hassan Mwinyi jijini Dar Salaam na uvumi wa chini chini kuenea kuwa baadhi ya wachezaji ‘walinunuliwa’ na mfadhili fulani aokoe hela alizowaahidi wachezaji kama wangetwaa Kombe.

Hata hivyo kinachotakiwa si kufika nusu fainali au fainali yenyewe, bali ni kutwaa kile kinachoshindaniwa (Kombe).

Yanga itacheza na Township Rollers ya Botswana saa 10:45 leo jioni kwenye mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mechi ya kwanza iliyochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, wageni kutoka Botswana waliiduwaza Yanga na mashabiki wao walipoifunga mabao 2-1.

Wakati Yanga wakicheza majira ya jioni, baada ya kuadhiriwa nyumbani, wenyeji wao watakuwa na ahueni kiasi kwa ushindi waliopata ugenini Dar es Salaam. Ni wazi kuwa Yanga watacheza kwa lengo la kupata ushindi wa haraka haraka ingawa wenyeji watacheza kwa kuzuia zaidi lango lao kutofikiwa na washambuliaji wa Yanga ili kulinda mabao 2-1 waliyopata jijini Dar es Salaam.

Simba wataingia uwanjani saa 2:30 usiku wa leo kupimana maarifa na wenyeji wao, Al Masry wa Misri jijini Cairo.

Ni mchezo utakaokuwa na ushindani wa vuta-nikuvute kutokana na timu hizo kufungana mabao 2-2 zilipokutana kwenye duru la kwanza jijini Dar es Salaam. Ilivyo ni kwamba Waarabu wana faida ya mabao mawili waliyofunga ugenini – Dar es Salaam – ingawa Simba nayo ilipata idadi kama hiyo.

Labda methali mbili zifuatazo zaweza kuwapa hamasa wachezaji wa Yanga na Simba ili wacheze kwa bidii na kuibuka na ushindi ugenini.

Mosi: “Mcheza hawi kiwete, ngoma yataka matao.” Matao ni mbwembwe na machachari. Maana yake mtu anayecheza ngoma hawi na kilema kwa kuwa uchezaji ngoma una machachari mengi.

Methali hii yaweza kuwanasihi wachezaji wa Yanga na Simba kuwa wadhamiriapo kupata ushindi, lazima wajitolee kufanya juhudi kubwa.

Hawapaswi kuwa na ulegevu au ajizi kwani ndiwo wanaoiwakilisha Tanzania. Ushindi wao ni sifa kwa Watanzania na nchi kwa jumla.

Pili: “Mcheza kwao hutuzwa.” Maana yake mtu anayecheza kwao hupewa zawadi au hutunzwa vizuri.

Hutumiwa kutufunza kwamba mtu anayefanya jambo lake vizuri au inavyopasa, hutuzwa au hupewa zawadi.

Hii ni tahadhari kwa Yanga na Simba kuwa zinapocheza nnje ya nchi, wananchi wa nchi hizo huzishangilia mno timu zao za nyumbani tofauti kabisa na sisi tunaozishangilia timu ngeni! Tahadhari hii yaihusu zaidi Simba kwani Waarabu wana mbinu nyingi za kuzidhoofisha timu ngeni zinapopambana na timu zao.

Kwa upande wa Yanga ambayo ina wakati mgumu zaidi, pia yapaswa kuwa makini kwani kwa mujibu ya magazeti ya michezo, Township Rollers ni timu inayopendwa sana Gaborone, jiji kuu la Botswana penye makazi ya Serikali.

Mengi yameandikwa na magazeti ya michezo nchini kuhusu mechi za leo.

Kadhalika viongozi mbalimbali wa vilabu vyetu wameeleza mengi kuhusu mechi hizo. Baadhi ya matajiri wameahidi kuwapa wachezaji fedha nyingi kama wakishinda.

Tahadhari kwa wachezaji wa Yanga na Simba: “Mbio za sakafuni huishia ukingoni.” Maana yake mbio za sakafuni humalizikia ukingoni.

Methali hii huweza kutumiliwa mtu anayejitia kufanya kazi fulani (kwa muktadha huu kandanda) kwa vishindo na makeke na hatimaye kushindwa kuimaliza kazi hiyo.

Wahenga walisema: “Jifya moja haliinjiki chungu.” Jifya ni jiwe mojawapo la kutelekea chungu. Mengi huitwa mafya. Maana yake mtu hawezi kubandika chungu juu ya meko yenye figa moja. Lazima yawepo mafiga matatu ndipo chungu kiweze kukaa vizuri.

Methali hii hutumiwa kuwashauri watu washirikiane katika shughuli zozote wazifanyazo. Hamna mtu anayeweza kufanya mambo yoyote yakafana bila kuwategemea watu wengine.

Kwa hiyo wachezaji wa Yanga na Simba leo wacheze kwa ushirikiano mzuri kwa lengo la ushindi na si vinginevyo. Wakumbuke kuwa penye nia pana njia nasi twaomba iwe hivyo.

Wakati hayo yakitokea huko, hapa nyumbani twasubiri kwa hamu yale maneno ya ‘wa kimataifa’ na ‘wa mchangani! Timu ipi itathibitisha maneno hayo leo? Yetu macho na masikio.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad