Klabu ya soka ya Simba imalazimishwa sare nyumbani na timu ya Al Masry ya Misri kwenye mchezo uliomalizika muda mfupi uliopita kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Mchezo huo ulikuwa na ushindani tangu dakika za mwanzo baada ya Simba kupachika bao la kuongoza dakika ya 9 kupitia kwa John Bocco kwa mkwaju wa Penalti baada ya mlinzi wa Al Masry kuunawa mpira.
Dakika ya 11 Al Masry walisawazisha kupitia kwa Ahmed aliyefunga kwa jitihada binafsi kufuatia walinzi wa Simba kufanya makosa kwenye eneo la hatari. Dakika ya 26 Al Masry waliongeza bao kupitia kwa Abdalrauf aliyefunga kwa penalti baada ya James Kotei kuunawa mpira.
Kipindi cha pili Simba walijitahidi kushambulia ambapo dakika ya 74 mshambuliaji Okwi alifanikiwa kuipangua ngome ya Al Masry kabla ya mlinzi mmoja kuunawa na Simba kupata penalti ambayo ilipigwa na Okwi na kuisawazishia Simba.
Baada ya Okwi kufunga bao la kusawazisha, Mvua kubwa ikanyesha jijini Dar es salaam hali iliyosababisha umeme kukatika na taa kuzimika kwenye uwanja wa taifa hivyo mechi kusimama kwa muda kabla ya hali kuwa shwari na mechi kuendelea, ambapo mechi imeisha kwa sare ya 2-2.