Utafiti uliofanywa na taasisi ya TWAWEZA na kuripotiwa leo Machi 29, 2018 umedai kuwa asilimia 80 ya wananchi wanataka wawe huru kumkosoa Rais katika mambo ambayo anafanya ndani ya nchi.
Katika utafiti huo ambao umeonyesha kuwa asilimia 70 ya Watanzania wamekuwa wakiamini zaidi kauli zinazotolewa na Rais John Pombe Magufuli wamehitaji kuwa huru pia kukosoa kauli hizo, asilimia 60 wanasema hawako huru kukosoa kauli zinazotolewa na Rais wakati asilimia 54 wanasema hivyo kuhusu kauli zinazotolewa na Makamu wa Rais na asilimi 51 kwa kauli za Waziri Mkuu.
Aidha utafiti huo umekwenda mbali zaidi na kuonyesha kuwa wananchi wanajisikia huru kuwakosoa Wenyeviti wa Vijiji, mitaaa na viongozi wa upinzani pamoja na madiwani
"Wananchi 8 kati ya 10 wanasema wanajisikia huru kuwakosoa mwenyeviti wa vijiji/mitaa (83%), viongozi wa vyama vya upinzani (77%), madiwani (76%)." alisema taarifa ya TWAWEZA
Mbali na hilo Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbas amefunguka juu ya utafiti huo na kusema kuwa yeye amekuwa akimshauri Rais John Pombe Magufuli na amekuwa akishaurika hivyo anashangaa kuona watu wanasema Rais hashauriki na kudai kuwa kuna njia ya kumkosoa Rais.
"Rais ni mtu mkubwa sana hata kumkosoa kunahitaji taratibu fulani. Kwenye familia unaweza kumkosoa kaka lakini baba huwezi kumwambia 'umebugi' mimi huwa namshauri Rais na ananisikia, wanaosema hashauriki wanamshauri wapi? alihoji Dkt. Abbas