Usajili wa Laini za Simu kwa Alama za Vidole Kuwashikisha Adabu Wanaotumia Mawasiliano Vibaya

Usajili wa Laini za Simu kwa Alama za Vidole  Kuwashikisha Adabu Wanaotumia Mawasiliano Vibaya
Serikali imezindua mfumo wa kusajili laini za simu kwa kutumia alama za vidole (biometria), ambao utadhibiti changamoto za usajili zilizopo.


Changamoto hizo ni pamoja na udanganyifu unaofanyika sasa kwa kutumia laini za sasa, sambamba na kuisaidia serikali kuwa na takwimu sahihi ya watumiaji wa huduma za simu za mkononi, zitakazosaidia kuweka mipango ya uchumi wa Taifa.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Mawasiliano, Dk Maria Sasabo, Mwakilishi kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Kitolina Kippa, alisema usajili wa laini za simu kwa kidole, utafanyika kwa majaribio katika mikoa sita nchini. Alisema pamoja na kuwepo matumizi sahihi ya simu za mkononi, lakini bado kuna watumiaji wachache ambao wanatumia huduma za mawasiliano vibaya. “Hawa wanatumia mianya katika usajili wa laini za simu kujipatia laini ambazo zimesajiliwa kwa majina bandia au ambazo hazijasajiliwa.

Wapo wanaotumia simu za mkononi kutuma ujumbe wa kashfa, matusi, kejeli, maudhi, dhihaka na unyanyapaa,” alisema. Alisema mfumo huo wa usajili ni hatua muhimu ya matumizi ya teknolojia katika kudhibiti changamoto za usajili na kuwezesha watoa huduma, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na serikali kuwa na takwimu sahihi za watumiaji wa huduma za simu za mkononi na vifaa vingine vya mawasiliano vinavyotumia laini za simu. Pia alisema kuwepo kumbukumbu sahihi za laini za simu, kutafanikisha kuanzishwa na kuwekwa kwa Kanzi Data ya laini za simu zilizosajiliwa ambayo inatakiwa na TCRA.

“Usajili sahihi pia ni muhimu kwa watumiaji wa huduma na wateja wa bidhaa kujihakikishia usalama wa kutotapeliwa au kuibiwa mitandaoni. Usajili wa laini za simu unawalinda watumiaji dhidi ya wahalifu wanaotumia mitandao,” alisema. Alisema; “Serikali tunafurahi tunapoona na kushuhudia ubunifu na utekelezaji wa mipango ambayo inalenga kuhakikisha maendeleo ya sekta na uchumi wa nchi kwa ujumla na ambayo inawahakikishia wananchi usalama wao na faida za kiuchumi na kijamii wanapotumia mitandao ya simu,” alisema.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba alisema kuwa mfumo huo wa usajili wa kutumia biometria umeanza kwa majaribio katika mikoa sita ikiwemo Dar es Salaam, Pwani, Iringa, Tanga, Singida na Mjini Magharibi na watakapokamilisha wataendelea na mikoa mingine. “Ili kukabiliana na changamoto za usajili, TCRA, watoa huduma za simu za mkononi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) tuliazimia kuja na mfumo huu wa usajili wa laini za simu hapa nchini ili kuepuka udanganyifu na kudhibiti uhalifu,” alisema.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad