Vigogo Mbaroni kwa Wizi wa Maji

Vigogo Mbaroni kwa Wizi wa Maji
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso amefanya ziara ya kustukiza katika Kiwanda cha Nguo cha 21st Century kilichopo mjini Morogoro na kuamuru kukamatwa kwa viongozi wake baada ya kubaini kuwa kiwanda hicho kinahujumu mapato ya Serikali kwa kuondoa mita inayorekodi matumizi ya maji nyakati ya usiku.



Mita hiyo iliyoondolewa na hivyo kufanya maji yatumike bila kujulikana kiwango cha matumizi hali ambayo imekuwa ikiikoseshamapato halali Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Manispaa ya Morogoro (Moruwasa). Waliotiwa mbaroni ni pamoja na Meneja Uzalishaji wa kiwanda hicho, Clement Munisi, Meneja wa Fedha Jayesh Vajdya pamoja na Msoma mita wa kiwanda aliyejulikana kwa jina moja la Samuel.

Naibu Waziri huyo, alisema amefanya ziara hiyo ya kustukiza katika kiwanda hicho baada ya kupata taarifa kutoka wasamaria wema kuwa nyakati za usiku vinafanyika vitendo vya hujuma kwa kuondoa mita hiyo ili maji yatumike bila kupimwa kiwango chake cha matumizi na kisha kuirudishia nyakati za asubuhi.

Alisema kuwa licha ya Serikali ya awamu ya tano kujali uwekezaji wa viwanda lakini viwanda hivyo vinaenda kinyume kwa kuunganisha maji kwa njia isiyo sahihi na kwamba vinapaswa kulipa gharama za matumizi yake ili fedha hizo ziweze kuendelea kutoa huduma katika maeneo mengine si kuhujumu jitihada za Serikali za kuwapa maji kwa ajili ya matumizi ya uzalishaji.

Aliamuru viongozi hao kukamatwa mara moja na kwenda kuhojiwa na vyombo vya ulinzi na usalama na kisha kufikishwa mahakamani mara moja kwa kitendo cha kuhujumu mali za serikali. Naibu waziri alisema kuwa baada ya kukamatwa kwa viongozi hao na kutoa maelezo wanapaswa kupigiwa hesabu kulingana na wizi huo na kuunganishiwa faini. Hata hivyo alisema kuwa, wizara hiyo imeanza kazi ya kupambana na watu wote wanaohujumu miundombinu ya maji na wizi iwe kwa mtu mmojammoja au taasisi na viwanda lengo ni kuongeza makusanyo ya mapato yatakayochangia kuendeleza miradi mipya ya maji.

Akielezea jinsi walivyobaini hujuma hizo, mkuu wa kuzuia upotevu wa maji wa Moruwasa, Bertam Minde alisema alisema walibaini hujuma hizo kwa muda mrefu na kubadilisha mita tatu tofauti huku wakifanya ukaguzi wa mita hiyo nyakati za usiku. Alisema kuwa juzi (Machi 10, mwaka huu) walifanya ukaguzi mchana na kuona kiasi cha maji kilichotumika ni uniti 977 na walipofika usiku waliosoma tena wakati kiwanda hicho kikiendelea na kazi na kukuta uniti 984 huku mita yake ikiwa imefunguliwa na kuwekwa pembeni.

Mkurugenzi wa Moruwasa, Nicholaus Angumbwike alisema kuwa walianza kufanya uchunguzi kwa kipindi cha miezi mitatu baada ya kuona malipo ya kiwanda hicho yamepungua gafla kutoka Sh milioni 80 kwa mwezi hadi kufikia Sh milioni 20 wakati matumizi ya maji katika mitambo yao yakionesha ni juu. Mhandisi Angumbwike alisema waliamua kuwafungia mashine maalumu kabla ya mita inayoonesha kiwango cha matumizi ya maji yanayoelekea ndani ya kiwanda hicho pamoja na mita mpya na kusoma mara kwa mara mita hiyo na kubaini mita hiyo imekuwa ikifunguliwa nyakati za usiku.

Alisema kuwa kabla ya kufunga mita hizo waliwataarifu uongozi wa kiwanda hicho kuwa wawe makini na mita hizo mpya zilizofungwa na zitakuwa zikifanyiwa ukaguzi wa mara kwa mara lakini kiwanda hicho kiliendelea na wizi wa maji. Mwanasheria wa Moruwasa, Tumaini Kimaro alisema kuwa kitendo kilichofanywa na kiwanda hicho ni kosa la uhujumu uchumi na wizi wa mali za serikali na wanapaswa kufikishwa mahakamani kwa kosa hilo. Meneja uzalishaji wa Kiwanda hicho, Clement Munisi alisema bomba hilo ni mali ya kiwanda hicho na kama kweli mita imetolewa ni hujuma kwa mali za serikali ila hajui aliyefanya kitendo hicho.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad