Tume ya mawasiliano nchini Uganda, UCC, imefungia zaidi ya vituo 20 vya redio vya FM.
Vituo hivyo vinashutumiwa kutangaza 'uganga wa kienyeji na kuwatapeli wananchi.'
Hatua hii inafuata onyo la tangu zamani viache kuwaweka hewani waganga wa kienyeji.
Tangazo hilo la kufungiwa vituo vya redio 23 limetolewa jana jioni na mwenyekiti wa Tume ya Mawasiliano Godfrey Mutabazi.
Bwana Mutabazi ameshutumu redio hizo kutumiwa na waganga wa kienyeji kuwatapeli wananchi na kuvunja sheria ya uchawi ya kifungu cha pili.
Redio hizo zimekuwa zikiwapa vipindi waganga hao wa kienyeji kutangaza uganga wao, huku wakiwaambia wananchi kutuma fedha kupitia njia ya simu za mikononi.
Msemaji wa tume ya mawasiliano Pamela Ankunda ameielezea BBC kuwa, "Kwa kuwaweka hewani matapeli wanaojiita waganga wa kinyeji, wakitumia mbinu mbali mbali wakiwa hewani ili kuwatepeli wananchi."
"Kwa mfano kwa kuwalaghia wananchI kwamba ukituma fedha hizo kwa njia ya simu ya mkononi utapata utajiri, baada ya kutuma kesho yake utapata mamilioni ya fedha chini ya kitanda chako.Hivyo tumetumia sheria ya kuwajibisha radio hizo na kufunga FM Radio 23 baada ya kusikiliza matangazo hayo." amesema Bi Ankunda
Baadhi ya vituo hivyo 23 ni kutoka wilaya mbalimbali zikiwemo redio mbili za jiji Kamapla ambazo ni Metro FM, Dembe FM inayomilikiwa na gazeti la Monitor, nyingine ni kutoka sehemu mbalimbali za nchi mashariki , kaskazini na magaharibi mwa Uganda.
Tume imewataka wamiliki wa redio zote zilizofungiwa kufika katika tume ya mamlaka ya mawasiliano ya kieloktroniki, inayohusika na kutoa leseni ya matangazo.
Bi Ankunda amesema vituo hivyo vina nafasi ya kufunguliwa wakifuata sheria.
"Bado wananafasi ya kuzungumza na tume, kama wakiandika barua ya kuomba msamaha na kuthibitisha kwamba hawatatangaza tena matangazo hayo na kufuata kanuni na sheria ya utangazaji, tutawarudisha tena hewani.
Hii siyo mara ya kwanza tume ya mamlaka ya mawasiliano kufungia redio za FM kwa kuvunja kanuni na sheria ya utangazaji nchini Uganda.
Miaka ya nyuma Rais Museveni amewahi kutishia kufungia vituo vya redio na pia kumekuwa na matukio ya polisi kuvamia baadhi ya vituo vya habari.